Friday, July 13, 2018

#WC2018: Viungo kuiteka fainali Ufaransa, Croatia

 

By Charles Abel, Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ubora wa safu ya kiungo kwa timu za Ufaransa na Croatia ni moja ya sababu zilizochangia timu hizo kutinga fainali ya Kombe la Dunia itakayochezwa keshokutwa mjini Moscow, Russia.

Uwezo mkubwa ulioonyeshwa na wachezaji wa viungo wa miamba hiyo kutibua mipango ya wapinzani na kuchezesha timu, kumezifanya kutawala mchezo na kupata ushindi kwenye mechi sita walizocheza kabla ya kufuzu fainali.

Takwimu za timu hizo katika michezo iliyopita zinaonyesha katika mechi zote za nyuma kabla ya kufuzu fainali, Ufaransa imekuwa na umiliki wa mpira wastani wa asilimia 51 na Croatia 56 kuanzia hatua ya makundi hadi nusu fainali.

Dalili za mchezo wa fainali baina ya timu hizo kutotabirika, zimeanza kuonekana mapema kutokana na ufanisi wa idara mbalimbali ndani ya uwanja ulioonyeshwa katika michezo iliyopita.

Timu hizo zimekuwa na uimara na udhaifu kwenye maeneo tofauti ndani ya uwanja ambao unaweza kuwa chanzo cha mojawapo kuibuka na ushindi na nyingine kukosa ubingwa.

Ufaransa imekuwa moto wa kuotea mbali kwa mashambulizi ya kushtukiza, ingawa imekuwa haitengenezi idadi kubwa ya nafasi zinazoweza kuifanya ifunge mabao ya kutosha yanayoweza kumaliza mchezo mapema.

Changamoto nyingine inayoikabili Ufaransa ni kukata pumzi katika dakika 15 za mwisho za kipindi cha pili jambo ambalo limekuwa likiiweka kwenye wakati mgumu katika mechi zake ingawa ilinusurika na kupenya hadi fainali.

Kwa upande wa Croatia imekuwa tishio na kipenzi cha idadi kubwa ya mashabiki kwa mfumo wake wa soka la pasi na kufungua uwanja, ambao umekuwa mwiba kwa timu pinzani kupata matokeo dhidi yao.

Soka limeifanya Croatia kuwa miongoni mwa timu zilizopiga pasi nyingi kwenye fainali hizo kwani imepiga 3,291 na sahihi zikiwa 2,660 wakati Ufaransa imepiga pasi 2,769 kati ya hizo 2,295 zilifika kwa walengwa.

Timu hiyo ambayo imeingia fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, imekuwa na tatizo la kucheza taratibu dakika za mwanzo za mchezo, udhaifu ambao Ufaransa inaweza kuutumia kufunga mabao ya mapema na kumaliza mchezo.

Hata hivyo, Ufaransa hasa safu yake ya ulinzi inapaswa kuwa makini na nyota wa Croatia ambao hawana mzaha wanaposogelea lango la timu pinzani.

Hadi inafika hatua ya fainali, Croatia imepiga mashuti 99 ingawa Ufaransa inaonekana sio timu inayopendelea kupiga mashuti mara kwa mara kwa kuwa imefanya hivyo mara 74 tu.

Kwa pamoja zimekuwa ni miongoni mwa timu zenye safu nzuri ya ushambuliaji hasa Croatia ambayo imefunga mabao 12 na Ufaransa ikifumania nyavu mara 10.

Hata hivyo, timu hizo haziko imara kwenye safu ya ulinzi na nyavu za Ufaransa zikiwa zimetikiswa mara nne na wapinzani wao zimeruhusu mabao matano.

Endapo Ufaransa itakuwa makini katika upigaji wa mipira ‘iliyokufa’, huenda ikapata bahati ya mtende kwenye fainali kutokana na udhaifu wa wapinzani wao wa kusababisha faulo za mara kwa mara.

Croatia hadi inafika fainali, imecheza faulo 99 na Ufaransa imetenda madhambi mara 74 tu.

Rekodi hiyo ya faulo inatoa picha ya wazi kwamba fainali hiyo inakutanisha timu ambazo hazina mwenendo mzuri wa nidhamu na kuthibitisha hilo, hadi sasa Croatia imeonyeshwa kadi 14 za njano na Ufaransa 10.

Kocha wa Azam, Mholanzi Hans van der Pluijm aliliambia gazeti hili kuwa mchezo huo utakuwa ni moja kati ya mechi ngumu za fainali kuwahi kuchezwa kwenye Kombe la Dunia.

“Croatia haipewi nafasi kubwa kwenye mashindano haya, lakini kiuhalisia ina kikosi kizuri na imara zaidi kinachoundwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye kiwango bora duniani.

“Ukitazama Ufaransa pia ina wachezaji bora wanaoweza kuamua mchezo muda wowote. Nadhani timu zote zimestahili kutinga hatua ya fainali na sitashangazwa na matokeo yoyote kwa sababu siku hizi hakuna timu ndogo,” alisema Pluijm. Mchezo wa kusaka mshindi wa tatu baina ya England na Ubelgiji utapigwa kesho. Katika mechi ya kwanza Ubelgiji ilishinda 1-0.

-->