Wednesday, March 27, 2013

Azam yapaa, Simba yaloa

Mshambuliaji wa Azam, Kipre Tchetche (chini)

Mshambuliaji wa Azam, Kipre Tchetche (chini) akiangukiwa na mwenzake John Bocco (juu) baada ya kufanyiwa faulo na beki wa Tanzania Prisons, Laulia Mpalile (kushoto) wakati wa mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jana. Azam ilishinda 3-0. Picha na Michael Matemanga 

By Jessca Nangawe na Vicky Kimaro, Mwananchi

Dar na Kagera. Azam imeendelea kujihakikishia nafasi ya kucheza mashindano ya Afrika mwakani baada ya kuichapa Prisons 3-0, wakati Simba ikinyukwa bao 1-0 na wachezaji 10 wa Kagera Sugar katika mechi za Ligi Kuu Bara.


Wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika CAF, Azam wakiwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex walipata ushindi huo na kufikisha pointi 40 na kuicha Simba kwa pointi sita na kuwa nyuma ya vinara Yanga kwa pointi nane.


Kiungo Kipre Balou aliifungia Azam bao la kwanza katika dakika ya 19, akiunganisha krosi ya Hamisi Mcha, naye mfungaji bora msimu uliopita, John Bocco aliifungia Azam bao la pili dakika ya 75 akiunganisha pasi ya Kipre Tchetche kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Prisons, David Burhan na kujaa wavuni.


Uzembe wa mabeki wa Prisons ulitoa zawadi kwa Tchetche kufunga bao la tatu kwa shuti akiwa yeye na kipa Burhan katika dakika ya 86.


Kagera: Jahazi la mabingwa watetezi Simba limezidi kuzama baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji wao Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Bao pekee la Kagera lilifungwa na Amandus Nesta katika dakika ya 46, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Salum Kanoni. Katika mechi hiyo mchezaji wa Kagera, Juma Nade alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Mrisho Ngassa katika dakika ya 90.


Pia katika mchezo huo Simba walifika golini kwa Kagera Sugar kwa mara ya kwanza katika dakika ya 62 kupitia mshambuliaji wake Ramadhan Salum, lakini shuti lake lilidakwa na kipa Andrew Ntala.


Vilevile nahodha wa Simba, Juma Kaseja alifanya kazi ya ziada kuinusuru timu yake kupata kipigo kikubwa kwa kuzuia mashambulizi mengi langoni mwake.
Wenyeji Kagera wanaofundishwa na Abdallah Kibaden walionekana kuwa bora zaidi katika sehemu kubwa ya mchezo katika mechi hiyo.

-->