Arsene Wenger mwisho wa enzi

Muktasari:

  • Wenger ametangaza kustaafu kuifundisha Arsenal mwisho wa msimu huu baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa miaka 22.

London, England. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alianza maisha yake England kwenye Uwanja wa Ewood Park dhidi ya Blackburn Rovers Oktoba 12,1996 hatimaye jana ametangaza kustaafu kuifundisha Arsenal.

Wenger ametangaza kustaafu kuifundisha Arsenal mwisho wa msimu huu baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa miaka 22.

Mfaransa huyo ataondoka katika klabu hapo mwaka mmoja kabla ya kumalizika kwa mkataba wake wa sasa.

“Nashukuru kupata nafasi ya kuifundisha klabu hii kwa miaka mingi yenye kumbukumbu,” alisema Wenger. “Nimeiongoza klabu hii kwa kujitoa kwa moyo wangu wote na akili yangu.

“Kwa wote wanaopenda Arsenal, kuchukua jukumu la kulinda heshima ya klabu hii.”

Mmiliki mkubwa wa Arsenal, Stan Kroenke alisema uamuzi huo wa leo Ijumaa kuwa “ni moja ya siku ngumu kwa wadau wa michezo baada ya miaka yote.”

Aliongeza: “Mmoja ya sababu kuingia Arsenal tulikuwa tukitaka Arsene kuipa mafanikio klabu hii ndani na nje ya uwanja.

Wenger aliziteka nyoyo za mashabiki wa Arsenal baada ya kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu England, Kombe la FA mara saba na Ngao ya Jamii mara sita, pamoja na kufanikisha klabu hiyo kuhama kutoka kwenye Uwanja wa Highbury kwenda Emirates mwaka 2006, hayo ni mafanikio yaliyopatikana katika miaka 22 ya Mfaransa huyo.

Wenger mwenye miaka 68, ambaye aliweka rekodi ya kutwaa vikombe viwili katika msimu mmoja aliposhinda ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA mwaka 1998 na 2002.

Hata hivyo, kwa sasa amewagawa mashabiki wa Arsenal, baada ya klabu hiyo kukaa miaka 14, bila ya ubingwa wa Ligi Kuu, lakini mchango wake katika soka la England umemfanya kuwa mmoja wa makocha wenye rekodi ya kipekee katika soka la sasa.

Wenger msimu wa 2003-04, alikuwa kocha wa kwanza tangu 1988-89 kuiongoza timu kucheza msimu wote bila ya kupoteza mchezo wowote.

Lakini baada ya kutwaa Kombe la FA 2005, ililazimika kusubiri miaka tisa mingine au siku 3,283 kupata taji lingine. Walipata taji hilo baada ya kuifunga Hull City na kutwaa Kombe la FA 2014, kabla ya kutwaa tena taji hilo msimu uliofuata.

Wenger alitwaa taji lake la saba la Kombe la FA msimu uliopita, baada ya kuifunga Chelsea mabao 2-1 kwenye Uwanja Wembley, lakini alimaliza katika Ligi Kuu akiwa nyuma kwa pointi 18 kwa vijana wa Antonio Conte waliotwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Kikosi chake kimekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika mashindano ya Ulaya tangu alipocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona mwaka 2006.

Arsenal imetolewa katika hatua 16 bora katika misimu saba mfululizo na msimu wa mwisho kucheza hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa 2017, walipofungwa 10-2 na Bayern Munich.

Mwaka 2006, walifanikiwa kuhamia kwenye Uwanja wa Emirates wenye thamani ya Pauni 390milioni wakitokea Highbury.

Gunners imekuwa na rekodi ya kufanya usajili wa gharama ndogo kulinganisha na wapinzani wake. lakini Wenger msimu huu amevunja rekodi ya uhamisho wa klabu hiyio mara mbili.

Alimnunua mshambuliaji Mfaransa Alexandre Lacazette kwa Pauni 46.5milioni pamoja na usajili wa mshambuliaji wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang wa Pauni 56milioni aliofanya Januari.