Taifa Cup yatua Arusha

Thursday December 7 2017

 

By Yohana Challe

Arusha: Mkoa wa Arusha umepewa dhamana ya kuwa wenyeji wa michuano ya netiboli ya Taifa Cup yanayotarajia kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki hii kwa kushirikisha timu za mikoa yote ya Bara.

Mwenyekiti wa Chaneta, Dk Devota Marwa alisema kuwa hadi sasa mikoa 11 tayari imethibitisha ushiriki wao katika michuano hiyo itakayofanyika kwa siku tisa kuanzia Desemba 10 hadi 19.

“Ratiba inaweze ikabadilika kulingana na uwingi au upungufu wa timu zitakazoshiriki kwa maana Mikoa mingine inaonekana kusuasua katika ushiriki wao kutokana na suala la fedha za kusafiria wachezaji kwenda kwenye mkoa husika wa mashindano licha ya Chaneta kughalimia malazi na chakula,” alisema Dk Marwa.

Hata Hivyo, Afisa Michezo wa Jiji la Arusha, Benson Maneno alisema kuwa taarifa alizopokea kutoka kwa uongozi wa mchezo huo wa mkoa kuwa tayari maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa ikiwa pamoja na timu ya Arusha kuwa tayari kwa mapambano.

“Arusha imekuwa na bahati kubwa kwa viongozi wa michezo wa juu kuupa mkoa wetu kipaumbele katika michezo kwani hata ligi ya mabingwa ya netiboli ilikuwa ifanyike hapa kabla ya kuhamishiwa Kilimanjaro na pia ligi kuu ya wanawake ya soka inafanyika Arusha” alisema Maneno.

Maneno alisema kuwa hadi juzi alipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa netiboli kuwa mikoa 16 inaweza ikawa miongoni itakayokuja kupambana katika michuano hiyo.

 

 

Advertisement