Dunia simama nishuke: Boban kwa Yanga, Mbaraka Namungo

Muktasari:

  • Katika miaka ya karibu Tanzania imeshudia wachezaji wengi chipukizi wakishindwa kuthibisha ubora wao mbele ya wakongwe katika klabu Simba, Yanga na Azam

Dar es Salaam. Kuna jambo halipo sawa katika jamii yetu, wakati dunia ikishudia vijana wakishika hatamu kwetu ni tofauti ni wazee ndiyo wanatamalaki kila kona.

Wimbi hilo limeanza kuingia kwa kasi katika michezo soka katika msimu huu tumeshudia mambo mengi ya kushangaza jambo linalopaswa wadau wa soka kuanza jitathimini kwa hali hii.

Ukiangalia kwa jicho la kawaida unaweza usione tatizo, lakini kwa mtu makini kinachotokea sasa ni ishara mbaya kwa mwenendo wa soka la nchi hii.

Nimeangalia usajili wa klabu mbalimbali pamoja na nyota wanaotamba sasa katika Ligi Kuu utagundua sasa Tanzania imeshindwa kuibui wachezaji wapya chipukizi wenye vipaji.

Hivi karibuni nimesikia Yanga wanataka kumsajili Haruna Moshi ‘Boban’ ni jambo jema kwake lakini hapo hapo unasikia chipukizi kama Yohana Nkomola na Mbaraka Yusuph wanatolewa kwa mkopo Namungo FC ya daraja la kwanza.

Hiyo haitoshi leo Mrisho Ngassa, Thabani Kamusoko, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, Donald Ngoma, Pascal Wawa, Aggrey Morris ndiyo wachezaji wanaotamba.

Ukiangalia umri wa wachezaji hao na wengine wanaotamba kwa sasa hiyo taa ya hatari imewaka ni lazima TFF na wadau wa soka kukaa chini na kujiuliza wapi inapokwenda.

Haiwezekani Nkomola, Mbaraka, Adam Salamba, Mohamed Rashid, Marcel Kaheza, Mlipili, Waziri Junior, Joseph Mahundi, Peter Manyika, na Joseph Mwashiya wanashindwa kutamba katika klabu Simba, Yanga na Azam tunaona ni kawaidi hapa kuna tatizo.

Tatizo linaweza kuwa ni wachezaji wenyewe kutojitambua na kushindwa kutunza vipaji vyao jambo linalofanya washindwa kushindana na wakongwe.

Jambo lingine linaweza kuwa ni mfumo wetu umeshindwa kutoa nafasi kwa wachezaji wetu chipukizi kuonyesha uwezo wao.

Tatizo hili linapoachwa kwa muda mrefu madhara yake yataonekana kwa timu yetu ya taifa, kwa sababu watarudisha wakongwe hawa tutakapokutana na timu za wenzetu zilizoundwa na wachezaji chipukizi kinachofuata kila moja anakijua.

Duniani kwa sasa wanaotamba katika klabu kubwa ni wachezaji chipukizi Mbappe, Rashford na wengine, mfano mzuri ni kikosi cha timu ya taifa ya England ukiangalia kimeundwa na vijana watupu.

Vijana hao wameifanya England kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 na sasa fainali za Mataifa ya Ulaya 2019.

Tanzania isitegemee kupiga hatua katika soka la kimataifa hasa timu ya Taifa kwa kuwategemea hawa wakina Ngasa, Boban.