Eden Hazard awaponda mashabiki wa Chelsea

Muktasari:

Mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard amechukizwa na kitendo cha mashabiki wa timu hiyo kumtolea maneno ya ubaguzi mchezaji Raheem Sterling.

London, England. Sakata la ubaguzi kwa mchezaji Raheem Sterling, limechukua sura mpya baada ya nyota wa Chelsea, Eden Hazard kuwabwatukia mashabiki wa klabu hiyo.

Hazard alisema hakupendezwa na kitendo cha mashabiki wa klabu yake kumtolea maneno ya ubaguzi nyota huyo wa Manchester City.

Hazard alisema anamuunga mkono Sterling kwa kuwa ni mchezaji bora duniani na hakubaliani na vitendo vya ubaguzi wanavyofanyiwa wachezaji wenye asili ya Afrika.

“Kwangu Raheem ni mchezaji hodari, niko upande wake. Uchunguzi wa tukio hili unaendelea sijui nini kitaamuliwa, naamini waliofanya vitendo hivi siyo mashabiki,” alisema Hazard.

Mashabiki wa Chelsea walimbagua Sterling pembeni mwa uwanja alipokwenda kurusha mpira katika mchezo ambao Chelsea ilishinda mabao 2-0.

Nahodha huyo wa Ubelgiji, alisema mashabiki waliombagua Sterling siyo watu wa mpira na wanastahili adhabu.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola na Jurgen Klopp anayeinoa Liverpool wamelaani na kueleza masikitiko yao kwa tukio hilo.

Sakata la winga huyo wa kimataifa wa England limeibua mjadala mzito England, likiwaibua baadhi ya nyota wa zamani akiwemo Paul Ince na Rio Ferdinand wenye asili ya Afrika ambao wametaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya mashabiki wote waliohusika katika tukio hilo.