Fedha alizovuna bondia Hassan Mwakinyo hizi hapa

Muktasari:

  • Mwakinyo alimchapa Eggington katika raundi ya pili ya pambano la raundi 10 la uzito wa super welter, lililoacha mshituko kwa mashabiki wa ngumi nchini Uingereza Jumamosi iliyopita.

Dar es Salaam. Licha ya bondia Hassan Mwakinyo kuweka rekodi iliyoshitua dunia kwa kumchapa kwa ‘Technical Knock Out’ (TKO) bondia namba nane kwa ubora duniani, Sam Eggington, lakini amevuna Sh6.6 milioni.

Mwakinyo alimchapa Eggington katika raundi ya pili ya pambano la raundi 10 la uzito wa super welter, lililoacha mshituko kwa mashabiki wa ngumi nchini Uingereza Jumamosi iliyopita.

Bondia huyo ambaye anatarajiwa kuondoka leo Uingereza kurejea nchini, aliweka rekodi ya kumtandika mpinzani wake ngumi 96 ambazo 51 kati ya hizo alipiga raundi ya pili iliyompa ushindi.

Pamoja na kupata umaarufu huo, fedha aliyoingiza ukiigawa na ngumi alimzompiga mpinzani wake kila moja ina thamani ya Sh68,000.

Mwakinyo anaondoka Uingereza na dola 3,000 (zaidi ya Sh6.6 milioni) ambazo amelipwa kwa kucheza pambano la utangulizi lililomkutanisha Amir Khan dhidi ya Sam Vargas.

Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Don Chief Promotion iliyoshiriki kutafuta pambano hilo, Juma Ndambile alisema Mwakinyo alistahili kulipwa fedha hizo kwa kuwa hakuwa bondia maarufu hadi aliposhinda.

“Dau lake litapanda kwa sasa ni staa, lakini alipokwenda Uingereza alikwenda kama bondia wa kawaida ambaye alikuwa nafasi ya 174 kwenye viwango vya ubora, lakini sasa amepanda hadi nafasi ya 16 hivyo atacheza mapambano ya bei mbaya,” alisema Ndambile.

Bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka alisema dau alilopewa Mwakinyo ni sahihi kwa kuwa ndiyo fedha ambayo promota wa pambano hilo ambaye ni mshirika wa Ndambile, Coffie Azumah amekuwa akilipa. “Mimi nimeshapigana mapambano matatu chini ya Coffie, awali alinilipa dola 3,000, lililofuatia niliongezewa dola 1,000 zaidi na pambano jingine alinilipa dola 5,000.

“Hata hivyo nilipopigana na Phil Williams (kuwania ubingwa wa dunia WBF), nilipanda kwenye viwango vya dunia, kitendo cha kupanda na dau langu pia lilipanda hadi kufikia Euro 12,000.

“Hata Mwakinyo kwa kuwa ameshakuwa maarufu hawezi kupigana mapambano ya bei rahisi, lazima aanze kucheza kwa pesa ndefu, lakini nimpe tu angalizo asije kukurupuka katika mapambano atakayocheza, ajipange,” alisema Cheka.

Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe alisema Serikali inatarajia kumuandalia mapokezi kabambe bondia huyo mwenye miaka 23 anayetokea mkoani Tanga atakapowasili nchini.

“Alichofanya Mwakinyo ni heshima, mbali na mapokezi tutakayompa, pia tutakaa naye ili tuone namna ya kumsaidia na kumuandaa kimkakati aweze kufika mbali,” alisema Waziri Mwakyembe.

Mwakinyo mbali na pambano la Uingereza, aliwahi kukosa mkanda wa ubingwa wa dunia wa WBC mwaka jana aliponyimwa ushindi nchini Russia dhidi ya Lendrush Akopian licha ya kumaliza raundi zote 10 na mwenyeji kupewa ushindi katika uzito wa super feather

Pia bondia huyo ana mkanda wa ubingwa wa WBA Pan Afrika ambapo alimchapa bondia wa Botswana, Anthony Jarmann kwa TKO raundi ya saba katika pambano la raundi 10 lililopigwa Gaborone.