Giniki aeleza alivyopata medali Uholanzi

Muktasari:

  • Mwanariadha Emmanuel Giniki, ametwaa medali ya fedha katika mbio za kilomita 10 zilizofanyika mwishoni mwa wiki nchini Uholanzi. Giniki ameshika nafasi ya pili baada ya kuchuana vikali na wanariadha wanaotamba kimataifa duniani wakiwemo Wakenya watano.

Dar es Salaam. Baada ya kutwaa medali ya fedha Uholanzi mwanariadha wa timu ya Taifa, Emmanuel Giniki amesema haikuwa kazi nyepesi kupata mafanikio kwa kuwa alikutana na wanariadha nyota wanaotamba katika mbio za kimataifa duniani.

Giniki aliyekimbia dakika 27:37 na kumaliza mbio, alichuana vikali na Wakenya watano, Waganda wawili na Waholanzi 13 katika kundi la kwanza na kuibuka mshindi wa medali ya pili ya fedha kwenye mbio za kilomita 10 za Singelloop Utrecht.

"Haikuwa rahisi kutwaa medali, nilipambana dhidi ya magwiji wa mbio, Mtanzania nilikuwa peke yangu lakini sikuhofu wala kuonyesha uoga dhidi yao," alisema nyota huyo wa mbio ndefu za uwanjani na barabarani nchini.

Katika mbio hizo, Giniki aliachwa kwa sekunde 13 na bingwa raia wa Kenya, Davis Kiplagat aliyetumia dakika 27:24 kumaliza mbio huku Mkenya mwingine, Isaac Kipsang akihitimisha tatu bora akitumia dakika 27:40.

Kocha wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), ambayo ndiyo inamnoa Giniki, Shabani Hiki alisema mwanariadha huyo alipanga kuvunja rekodi ya muda wake kwenye mbio hizo.

"Giniki alipoondoka alituambia anakwenda kuchukua medali, kama ataikosa lazima avunje 'time' na amefanya vyote viwili kwa wakati mmoja," alisema Hiki.

Alisema mwanariadha huyo alitafutiwa mbio na meneja wake, Marc Corstjens baada ya mpango wa kuitwa timu ya Taifa iliyokuwa inakwenda Cardiff, Uingereza kwenye michezo ya Madola kukwama dakika za mwisho.

Baada ya ushindi huo, nyota huyo atakwenda Lisbon, Ureno kushiriki mashindano mengine ya kilomita 10 na atachuana tena Jumapili wiki hii kwenye mbio za Mijl Van Groningen Marathoni.

"Nimejiandaa kufanya vizuri pia kwenye mbio hizo, niko vizuri kimwili na mashindano, Watanzania nyumbani waendelee kuniombea na mimi sitawangusha," alisema Giniki.