Friday, October 13, 2017

Kocha Msaidizi Mwadui abwaga manyanga

 

By Saddam Sadick, Mwananchi ssadick@mwananchi.co.tz

Kocha msaidizi wa Mwadui FC,Khalid Adam amebwaga manyanga kwa madai ya kashfa ya kuwanunulia pombe wachezaji na kusababisha timu hiyo kufanya vibaya katika michezo yake ya Ligi Kuu Bara.

Mwadui kesho itashuka uwanjani kuivaa Azam kwenye uwanja wao wa nyumbani, haijapata matokeo mazuri kwani kwenye mechi tano walizocheza wamevuna pointi nne na kukaa nafasi ya 12.

Adam alisema kuwa ni jambo la kashfa mbaya kwake kushtumiwa na Mwenyekiti wa timu kumtuhumu yeye ndiye kikwazo ndani ya timu kutofanya vizuri na kwamba anawanunulia pombe wachezaji.

Alisema ameamua kuchukua uamuzi hyuo ikiwa ni kulinda heshima na taaluma yake na kwamba mtu mmoja hawezi kumhalibia maisha hivyo anawaachia timu yao.

 “Siwezi kuendelea na timu, kitendo cha Mwenyekiti kunishtumu kwamba ninawanunulia pombe wachezaji na kuwa chanzo cha timu kufanya vibaya mimi siwezi kabisa kuvumilia," alisema Adam.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Joseph Kaasa alisema kocha huyo hajaamua yeye kuondoka, isipokuwa ni mpango wa menejimenti kumfungia virago kutokana na mwenendo wake mbaya.

Alisema kuwa hataki kuelezea zaidi juu ya sababu za kumfukuza kupitia vyombo vya habari, isipokuwa ni moja ya mkakati wa timu kufanya mabadiliko ili iweze kufanya vizuri.

“Hajaamua yeye kuondoka, ni uongozi ambao umeamua kumuacha kutokana na mwenendo wake, sitaki kuelezea zaidi kupitia vyombo vya habari, ila huu ni mkakati wa mabadiliko ndani ya  timu ili ifanye vizuri,” alisema Kaasa.

 

-->