Katiba yawapiga kitanzi vigogo wapya Simba SC

Mulamu Nghambi.

Muktasari:

Nguvu na mamlaka makubwa kwa wajumbe sita watakaochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Simba utakaofanyika Novemba 3, ipo katika upangaji wa sera na mipango tofauti na awali ambapo walikuwa wakishiriki moja kwa moja shughuli za klabu.

Dar es Salaam. Wakati wadau 21 wakichukua fomu za kuwania nafasi sita za uongozi, Katiba ya Simba itawabana na kupunguza nguvu ya wajumbe watakaochaguliwa kujihusisha na utendaji kazi wa moja kwa moja ndani ya klabu hiyo tofauti na awali.

Nguvu na mamlaka makubwa kwa wajumbe sita watakaochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Simba utakaofanyika Novemba 3, ipo katika upangaji wa sera na mipango tofauti na awali ambapo walikuwa wakishiriki moja kwa moja shughuli za klabu.

Wajumbe hao sita ambao miongoni mwao kutakuwa na mwenyekiti, hawatakuwa na nguvu au mamlaka ya kuajiri wala kuiwajibisha sekretarieti ya klabu hiyo na hawataweza kuongoza kamati za ndani.

Kuondolewa kwa kamati mbalimbali ndani ya klabu hiyo na uanzishwaji wa idara mpya za kitaalamu na weledi chini ya muundo wa kampuni, ni miongoni mwa sababu kuu zitakazolazimisha wajumbe watakaochaguliwa kuishi upya tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya Simba kubadilisha mfumo wa uendeshaji.

Utendaji kazi wa kila siku wa Simba utafanywa na wataalamu watakaoajiriwa kuongoza idara mbalimbali tofauti na awali ambapo wajumbe wa iliyokuwa kamati ya utendaji walikuwa wasimamizi na watekelezaji wa baadhi ya majukumu.

Pia majukumu mengine ambayo wajumbe hao ambao hawatahusika nayo ni usimamizi wa uongozi wa kamati mbalimbali za muda ambazo zimefutwa.

Awali, Simba ilikuwa na kamati zikiwemo za soka la vijana, usajili, ufundi na mashindano ambazo kwa katiba ya zamani zilikuwa zikiongozwa na mjumbe wa kamati ya utendaji.

Kwa mujibu wa katiba mpya, mjumbe pekee ambaye angalau anaweza kuwa na mamlaka katika shughuli za klabu ni mwenyekiti ambaye amepewa mamlaka ya kuitisha na kuongoza mkutano mkuu na kuteua wajumbe wawili kuingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi Simba.

Kamati ambazo Katiba ya Simba inazitambua na zitaendelea kuwepo kisheria ni kamati ya nidhamu, maadili na uchaguzi.

Kamati hizo zitaongozwa na wajumbe watakaoteuliwa na kuchaguliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba.

Kwa mujibu wa Katiba ya Simba, wajumbe wa kamati hizo tatu, wanabanwa na wanalazimika kutokuwepo wala kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya klabu hiyo.

“Kimsingi watu waliochukua fomu za kuwania uongozi wanapaswa kufahamu hawatakuwa na kazi au majukumu mengine zaidi ya kupanga mipango ya kuhakikisha malengo yanafikiwa huku usimamizi na utekelezaji wake ukifanywa na wataalamu wa idara husika na sio vinginevyo.

“Yale masuala ya kamati hayatakuwepo tena kwa sababu Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) haliungi mkono kamati za namna hiyo.

“Maana yake ni kwamba Simba inakwenda kwenye mfumo wa weledi zaidi ambao hauna tena mambo ya ubabaishaji na ujanja ujanja,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kuratibu Mabadiliko ya Mfumo wa Uendeshaji Simba”, Mulamu Nghambi.

Septemba 2, Kamati ya Uchaguzi ya Simba chini ya Mwenyekiti Boniface Lyamwike ilitangaza siku 63 za mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Klabu utakaofanyika Novemba 3, mwaka huu.

Kutangazwa kwa mchakato huo kulikuwa ni muendelezo wa utekelezaji wa agizo la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) la kuitaka Simba ifanye uchaguzi, baada ya uongozi wa sasa kumaliza muda wake.

Mchakato huo ulianza kwa wagombea kuchukua fomu uliofanyika kwa siku nane kuanzia Septemba 3 hadi 10 ambapo wadau 21 walichukua fomu za kuwania nafasi ya mwenyekiti na ujumbe.

Wakati mwanasoka wa zamani wa Simba, Mtemi Ramadhani na mwanachama maarufu wa klabu hiyo Swedi Nkwabi wakijitokeza kuwania nafasi ya mwenyekiti, wadau 19 walijitokeza kuchukua fomu za kuwania ujumbe katika uchaguzi huo.

Wagombea waliochukua fomu ni Christopher Mwansasu, Dokta Zawadi Ally Kadunda, Abubakar Zebo, Patrick Rweyemamu, Hamis Mkoma, Ally Suru, Alfred Eliya na Omar Selemani.

Wengine waliojitokeza ni Mohamed Wandi, Juma Pinto, Said Tully, Mwina Kaduguda, Idd Kajuna, Hussein Mlinga, Jasmeen Badou na Mkurugenzi wa Bendi ya African Stars Asha Baraka.