Kifo kilivyokatisha ndoto ya Kaka kuirudisha Tukuyu Stars Ligi Kuu

Muktasari:

  • Mke wa Ramnik Patel 'Kaka' Neva Patel amesema kifo kimekatisha ndoto ya mmewe kuirejesha Tukuyu Stars kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara.Kaka aliyekuwa mfadhili mkuu wa Tukuyu Stars ya Mbeya inayoshiriki Ligi daraja la pili alifariki wiki iliyopita huku mkewe akisimulia namna alivyokuwa akifikiria kuipandisha timu hiyo iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1986 kabla ya kuteremka daraja msimu uliofuatia.

“Aisee! Ninashindwa nianze wapi maana kila muda tulipokuwa katika maongezi na mume wagu alisisitiza kuwa akipona lazima airejeshe Tukuyu Stars Ligi Kuu Tanzania Bara”.

Hivyo ndivyo mkewe Neva Patel anavyoianza simulizi fupi ya maisha ya aliyekuwa mfadhili mkuu wa klabu hiyo Ramnik Patel ‘Kaka’ siku zote walipokuwa katika mazungumzo yao alikuwa akisisitiza akipona lazima airudishe Tukuyu Stars Ligi Kuu.

Neva anasema katika enzi za uhai wake alikuwa anawaza soka, hata siku za karibuni alivyoanza kuzidiwa alisikitika kutokwenda uwanjani kuzishuhudia Yanga, Simba, Mbeya City na Prisons na Tukuyu stars ikicheza uwanja wa Sokoine.

“Ni pigo kwangu mimi na wadau wa Tukuyu Stars mwaka huu alikuwa anatamani awaone angalau wachezaji wa sasa”, anasema Neva.

Neva anaendelea kusema kuwa hata alivyopata taarifa kwamba Tukuyu Stars imepanda daraja la pili, alifurahi akimini ndoto yake ya kuirudisha timu hiyo katika mashindano ya Ligi Kuu itatimia.

Anasema Kaka alikuwa akikataa michango ya wadau wa michezo waliyokuwa wakimpa kama pole alivyokuwa amelazwa hospali na aliwataka wapewe viongozi wa klabu kusaidia timu zao.

Baadhi ya wachezaji nyota waliotamba Tukuyu Stars na kuipa ubingwa mwaka 1986 kabla ya kuteremka daraja msimu uliofuata ni Mbwana Makata, Justine Mtekele, Selemani Mathew, Godwin Aswile ‘Scania’, Jimmy Mored ‘Moro’, Steven Mussa na Sekilojo Chambua.

Wadau soka wanena

Mdau wa michezo Enock Mwatujobhe anasema mbali na klabu hiyo kuwa na wachezaji hodari, lakini mchango wa mfanyabiashara huyo marufu ulichangia Tukuyu Stars kufanya vizuri.

Mwatujobhe anasema Kaka ndiye aliyekuwa anahudumia mahitaji yote muhimu ya timu usafiri, malazi na chakula ilipokuwa kambini.

Naye Patrick Aloyce mkazi wa Tukuyu anasema, uwepo wa kaka katika timu hiyo, ulifanya klabu hiyo kuishi kifahari hata kuzizidi Simba na Yanga kutokana na mambo ambayo alikuwa akiifanyia Tukuyu Stars.

Mchambuzi wa soka Charles Makwaza anasema, makubwa aliyokuwa anayafanya Kaka kwa Tukuyu Stars yaliwafanya wachezaji wa timu nyingine kutamani ‘kukipiga’ katika klabu hiyo.

Mchezaji huyo wa Mecco anadokeza ingawa timu hiyo ilikuwa ikimilikiwa na kampuni lakini hawakuweza kufikia maisha mazuri waliyokuwa wakiishi mahasimu wao Tukuyu Stars.

Tukuyu Stars yamlilia

Mlezi wa sasa wa klabu hiyo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Julius Chalya, anasema ni pigo kwa wadau wa soka wilaya, mkoa na Taifa kwa kuwa Kama ameacha historia ya pekee.

“Kutambulika kwa Wilaya ya Rungwe na Mkoa wa Mbeya kiujumla kulitokana na Kaka kuipaisha Tukuyu Stars kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1986 na ndiyo timu iliyochukuwa ubingwa kwa kuzipiku Simba na Yanga zilizokuwa zimezoeleka.

“Naweza nikamuelezea Patel ni miongoni mwa watu maarufu ambao watakumbukwa wilayani Rungwe kupitia soka”, anasema Chalya.

Katibu Mkuu wa Tukuyu Stars, Godfrey Mkumbwa anasema wamepata pigo kuondokewa na Kaka kwa kuwa alikuwa ni mwanamichezo aliyependa maendeleo ya soka.

Tukuyu Stars ilianzishwa mwaka 1980 na kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu) 1986 na baada ya mwaka mmoja ilishuka daraja.

Mwaka 1988 ilirejea katika ushindani kabla ya kukutana na changamoto mbalimbali za kiuchumi iliyochangia timu hiyo kuporomoka hadi daraja la tatu.

Hata hivyo, uongozi wa Tukuyu Stars ulisimama imara na kufanikiwa kuirejesha Daraja la Pili mwaka huu na mkakati ni kuhahakisha inacheza kwa kiwango bora na kupanda Ligi Kuu.