Liverpool vs Man. United ni mpambano wa kibabe

LONDON, England. Shughuli ipo leo hapo Anfield. Miamba ya soka katika Ligi Kuu England, Liverpool itakuwa nyumbani kuikaribisha Manchester United katika mpambano mkali huku makocha wa pande zote wakijitanabahi kushinda.

Kocha Jürgen Klopp wa Liverpool anaonekana kuwa na presha zaidi kwani Manchester United huwa haitabiriki hasa inapokuwa haijatimia kwani nyota wake wengi ni majeruhi.

Tatizo ni kwamba watakaocheza wanaweza kushangaza kwa kuilaza Liverpool lakini presha ya Klopp pia ni kuvurugiwa rekodi yake ya kutofungwa hadi sasa.

Timu hizo zinakutana katika mpambano ambao kila upande una rekodi yake na Liverpool inaialika Man United inayotokea Barabara ya East Lancs ikiwa na shauku ya kuzoa pointi zote tatu katika mpambano huo.

Mechi hiyo itakayochezeshwa na mmoja wa waamuzi watata, Martin Atkinson, Klopp anaingiza timu akiwakosa baadhi ya nyota wake; Trent Alexander-Arnold, Gomez, Solanke na Joel Matip ambao ni majeruhi. Wiki iliyopita Joe Gomez aliongeza idadi ya wachezaji majeruhi.

Kwa msingi huo, Klopp atakuwa akiwategemea zaidi mabeki wa kati, Virgil van Dijk na Dejan Lovren.

Furaha yake ni kwa nyota wake, Nathaniel Clyne aliyekuwa majeruhi, amerudi kwenye ubora wake wakati James Milner anaweza kusimama upande wa kulia katika ngome.

Liverpool inayotumia mfumo wa 4-4-2, inaweza kupangwa hivi: Alisson; Milner, Robertson, Lovren, Van Dijk; Wijnaldum, Fabinho, Shaqiri, Keita; Salah na Firmino.

Naye kocha Mourinho kwa upande wake, matumaini yake yako kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi na sasa wamerudi na watashuka pale Anfield. Hata hivyo, mashine zake kadhaa zitakosekana; Marcos Rojo aliumia mechi ya Valencia na pia atawakosa Victor Lindelof na Alexis Sanchez.

Pia katika orodha nyingine, baadhi pia wako kwenye hatihati ya kucheza ni pamoja na; Chris Smalling, Diogo Dalot, Anthony Martial, Matteo Darmian, Luke Shaw na Scott McTominay.

David de Gea na Nemanja Matic, ambao walipumzishwa baada ya shughuli ya Valencia, Mourinho alisema atampanga De Gea langoni lakini utata bado uko kwa Paul Pogba, kama atampanga ama la kwani mechi na Valencia alicheza chini ya kiwango.

Manchester United inayotumia mfumo wa 4-2-3-1 inaweza kupangwa hivi; De Gea; Dalot, Young, Jones, Smalling; Matic, Pogba; Mata, Rashford, Lingard; Lukaku.