‘Mechi ‘lainilaini’ zimeilemaza Stars’

Kiungo wa Taifa Stars, Himid Mao akijaribu kumzuia mshambuliaji wa Algeria, Riyad Mahrez wakati timu hizo zilipokutana mjini Algiers, Algeria. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Taifa Stars ikiwa nchini Algeria, ilikimbizwa na kuchapwa mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Dar es Salam. Kucheza kwa kutokujiamini, kocha kushindwa kuwaita wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje na kuzoeshwa mechi laini kumetajwa ndiyo chanzo cha kufungwa na Algeria juzi mchezo wa kirafiki.

Taifa Stars ikiwa nchini Algeria, ilikimbizwa na kuchapwa mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Taifa Stars itacheza mchezo mwingine na DR Congo Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kipigo hicho kimeibua mjadala huku baadhi ya makocha wakisema kiwango cha Stars kimelemazwa na mechi nyepesi za kirafiki.

Wasemavyo makocha

“Matokeo hayo ndiyo tulistahili, Algeria sio ‘levo’ yetu kisoka na ili tufikie kwenye levo hiyo lazima tuendelee kucheza nao mara kwa mara.

“Hawa wachezaji wamelemaa na mechi za Burundi, Watanzania huwa tunaziona mechi kama ya jana ‘juzi’ ni kubwa kwetu tunapenda mteremko tucheze na Somalia, Djibouti, Burundi au Malawi ambazo nazo zinatutoa jasho,” alisema Jamhuri Kihwelu ‘Julio.

Alisema Watanzania wameponzwa na dhana kuwa Stars haina uwezo wa kucheza na timu kama Zambia, Cameroon, Misri, Ivory Coast, Ghana, Nigeria na Algeria.

Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibaden alisema: “Tatizo la Stars wanacheza na watu wa aina gani kwenye klabu zao na hata mashindano ya kimataifa ya kirafiki?,” alihoji Kibadeni na kuendelea.

“Mtazameni Samatta (Mbwana anayecheza Genk ya Ubelgiji) yuko fiti sababu alipitia TP Mazembe hivyo hata alipokwenda Ulaya haoni tabu sababu akiwa Mazembe amecheza mechi nyingi tafu.

“Vivyo hivyo Msuva (anacheza soka la kulipwa Morocco) amebadilika mno, sababu huko aliko soka linachezwa na kuna timu hizi hizi vigongo, binafsi ninaamini kama Stars itaendelea kucheza mechi ngumu kama ya jana (juzi) itafungwa ila baada ya muda itabadilika,” alisema Kibadeni.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk Mshindo Msolla alikuwa tofauti kidogo na wengine akihitaji mabadiliko kwenye benchi la ufundi.

“Unajua kama kocha ameshindwa kuiongoza timu kwenye mechi muhimu kama ya kufuzu CHAN, AFCON na Kombe la Dunia, maana yake mbinu zake sio.

“Ni sawa ameshinda katika mechi za Cosafa lakini hizo sio muhimu sana, tukubali au tukatae lakini tunahitaji mabadiliko kwenye benchi la ufundi.

Kocha wa Lipuli, Suleiman Matola alisema viwango vya wachezaji wa Stars sio vibovu kama ambavyo inadhaniwa lakini akaungana na makocha, Kibadeni na Julio kuwa mechi ya Algeria haikuwa kiwango chao.

Mchambuzi wa Soka, Ally Mayay alisema ubora wa Stars unashuka kutokana na wachezaji kukosa muendelezo.

“Kuna wachezaji ambao tulitarajia wawe kwenye piki kipindi hiki lakini imekuwa tofauti, wengi wao wameonekana kukosa uwezo, Mayanga alipaswa kufuatilia kiwango cha kila mchezaji kwenye klabu yake kabla ya kumwita Stars.

“Pia hata baadhi ya wachezaji wa Ngorongoro wangeanza kupewa nafasi Stars, kwani wachezaji kama Bocco (John), Yondani (Kelvin) wanaelekea ukingoni,” alisema.

Akizungumzia kiwango cha Mayanga, Mayay alisema mechi ya Algeria ilikuwa kubwa kwa Mayanga.

Hata hivyo, katika mahojiano na gazeti hili, kocha Mayanga alikiri kuzidiwa kimchezo lakini akasisitiza kipigo hicho kimetokana na makosa ya uwanjani.