Mrwanda: Umaskini kwa mchezaji kujitakia

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo amecheza soka la kulipwa na kutamba katika Ligi Kuu Vietnam

 Mshambuliaji mkongwe Danny Mrwanda amesema kwa mchezaji chipukizi anayecheza soka kwa malengo, hawezi kuwa maskini akitambua thamani yake, milango ya kufika mbali ipo wazi.

Mrwanda ametolewa kwa mkopo na  Majimaji ya Songea kwenda JKT Mlale, alisema ugumu wa kazi ya soka ni jinsi ambavyo mchezaji mwenyewe anavyoweka umakini katika mipango yake ya kufika mbali.

"Soka la sasa siyo la kificho, kuna mawakala wengi ambao wanaweza kuwa mwanga wa wachezaji kufika mbali, kinachotakiwa ni mchezaji kuwa makini kusimamia mkataba wake na kuheshimu kazi yake."

"Naamini soka ukiliheshimu, litakuheshimu lasivyo utaona umechagua kazi ya kijinga inayoshusha thamani yako mbele ya jamii inayokuzunguka, cha msingi ni kuepuka ulewa sifa,"alisema aliyewahi kucheza soka la kulipwa nchini Vietnam.