Mtibwa Sugar waanzishia tambo kwa Simba SC

Muktasari:

Sabato alisema kuwa timu hiyo ina kila msimu imekuwa ikiondokewa na wachezaji kadhaa muhimu wanaotwaliwa na timu nyingine lakini huwaibua wengine na kufanya makubwa.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Kelvin Sabato, amesema hawatishiki na Simba mechi yao Ngao ya Jamii licha ya kuondokewa na baadhi ya nyota wao.

Sabato alisema kuwa timu hiyo ina kila msimu imekuwa ikiondokewa na wachezaji kadhaa muhimu wanaotwaliwa na timu nyingine lakini huwaibua wengine na kufanya makubwa.

Mchezaji huyo alisema kuondoka kwa viungo Hassan Dilunga aliyejiunga na Simba na Mohammed Issa ‘Fei Toto’ aliyehamia Yanga, hakutaiteteresha Mtibwa Sugar.

“Mtibwa kila wanapoondoka wachezaji huibuliwa chipukizi kutoka timu yetu ya vijana na kufanya vizuri naamini hata msimu huu vijana watakaopandishwa watafanya mambo makubwa,” alisema Sabato huku akiwapa tambo kuwa wasitarajie mteremko.

Alisema kutokana na hilo anaamini kikosi chao kitafanya makubwa msimu huu tofauti na kile walichokifanya katika msimu uliopita kwa kuwa mbali ya kuwa na chipukizi walioonyesha uwezo mkubwa lakini wachezaji karibu wote wa kikosi cha kwanza watakuwepo.

“Katika mazoezi tunayoyafanya yanaonyesha dalili kuwa msimu huu tutakuwa na kikosi bora zaidi, sababu msimu huu hatujaondokewa na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza kama misimu iliyopita,” alisema.

Mtibwa walimaliza msimu uliopita vizuri kwa kutwaa ubingwa wa FA, hivyo kujikatia tiketi ya kucheza mechi ya ufunguzi wa msimu na kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika.

Katika mechi ya ufunguzi wa msimu, Mtibwa Sugar itashuka dimbani Agosti 18 kukipiga na Simba katika mechi ya ufunguzi wa msimu itakayofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, mchezo wa Ngao ya Jamii.

Baada ya mchezo huo wa ufunguzi, Mtibwa Sugar itajiandaa kuikaribisha Yanga, katika mchezo wa kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika Agosti 23, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.