Mwakyembe ampa tano mkalimani wa bondia Mwakinyo

Muktasari:

  • Mafanikio ya bondia huyo yamemuingiza katika anga za mabondia maarufu duniani Athony Joshua wa Uingereza na Manny Pacquiao anayetokea Philippines.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamadumi na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amepongeza Mkalimani wa bondia Hassan Mwakinyo akisisitiza alichokifanya ni sahihi.

Baada ya ushindi wa Mtanzania huyo alipopata nafasi ya kuzungumza na vyombo vya habari mkalimani Rashid Nasoro aliyekuwa match maker wa pambano hilo hapa nchini kutokana na kutafisiri tofauti na kile alichokuwa akisema Mwakinyo.

Nassoro ‘Chid’ ni miongoni mwa mapromota wa ngumi nchini aliyewahi kuwa bondia wa kulipwa lakini hakuvuma aliteka hisia za watu wengi kwa jinsi alivyokuwa akipotosha kile alichokuwa akisema mshindi huyo.

Akizungumzia sakata hilo waziri Mwakyembe alisema Mwakinyo hakupaswa kujieleza kwamba anaishi maisha magumu, huo ni unyonge tena kwa bondia ambaye tayari aliweka rekodi kubwa namna ile, hivyo mkalimani amefanya sawa sawa.

Mwakyembe alisema Serikali itamsaidia katika mkakati wake wa kujiandaa na mapambano mengine.

“Atakapofika nchini tutakaa naye kujua tunamsaidia vipi katika pambano lake la Ujerumani, lazima tumsaidie, sasa hivi atakuwa akiangaliwa na mabondia wakubwa zaidi lakini ili afike mbali, lazima twende kimkakati.

“Tujipange tumsaidie aweze kuendeleza rekodi zaidi ili kuwa bingwa mkubwa wa dunia na kuipa heshima nchi na yeye kunufaika kwa kipaji chake,” alisema Waziri Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema Mwakinyo ni matunda ya Serikali kuingilia kati kumaliza vurugu zilizokuwepo muda mrefu kwenye ngumi za kulipwa.

Mwakinyo ameweka rekodi kwa kuingia katika orodha ya kuwa bondia namba 16 kwa viwango vya ubora duniani.

Mwakinyo ameweka rekodi muda mfupi baada ya kumdunda kwa TKO bondia wa Uingereza, Sam Eggington katika pambano la uzito wa super welter.

Mafanikio ya bondia huyo yamemuingiza katika anga za mabondia maarufu duniani Athony Joshua wa Uingereza na Manny Pacquiao anayetokea Philippines.

Hii ni mara ya kwanza kwa bondia wa Tanzania kupata mafanikio makubwa katika medani ya ngumi duniani.

Mwakinyo ambaye ni mkazi wa mkoani Tanga, ameishangaza dunia baada ya kumchakaza mpinzani wake katika pambano lililokuwa la utangulizi baina ya Amir Khan dhidi ya Samuel Vargas.

Baada ya ushindi huo, Mwakinyo ameingia kwenye rekodi akiwa bondia pekee wa Afrika aliyeingia kwenye orodha ya mabondia 50 bora wa dunia katika uzito wa super welter.

Ushindi wa ‘Technical Knock Out’ (TKO) wa raundi ya pili dhidi ya mpinzani wake anayeshika nafasi ya nane kwa ubora duniani umeitangaza vyema Tanzania katika mchezo wa masumbwi.

Wakati Mwakinyo akipanda, mpinzani wake ameporomoka hadi nafasi ya 30 kwa viwango vya ubora duniani.

Mwakinyo amepata nyota nne na nusu katika ubora wa ngumi na anakaribia kuingia katika rekodi ya bondia namba moja wa dunia kwenye uzito huo Jarett Hurd raia wa Marekani ambaye ana nyota tano.

Idadi hiyo ni sawa na ile ya nguli  wa uzito wa juu duniani raia wa Uingereza Joshua na Pacquiao  ambao pia wana nyota tano kila mmoja.

Rekodi ya Mwakinyo iliyoacha mshituko Uingereza imempa fursa ya kuandaliwa pambano la kuwania ubingwa wa Kimataifa wa IBF kwa vijana litakalopigwa Oktoba 20 Ujerumani dhidi ya Wanik Awdijan.

 

Wadau wafunguka

Mbali na kauli ya Serikali, kocha wa zamani wa timu ya Taifa, Nassor Michael alisema Mwakinyo ana nafasi ya kuwa bondia bora duniani kama Joshua endapo atapata msingi mzuri kuanzia sasa.

“Kinachohitajika ni maandalizi, anapaswa kuwa na kocha mwenye kiwango bora, ikiwezekana atakaporejea nchini kutoka Uingereza aanze kambi mapema kujiandaa na pambano la Oktoba,” alisema Michael aliyewahi kuwa kocha wa timu ya Taifa iliyofuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008.

Michael alimtaka bondia huyo kuongeza uzito wa ngumi anazorusha kwa sababu kwa kuwa atakutana na mabondia hodari duniani.

Bondia Amos Mwamakula alisema kuwa Mwakinyo anahitaji kuungwa mkono na Serikali wakati akijiandaa na pambano jingine la Ujerumani.

“Mwakinyo sasa sio bondia wa ‘uswahilini’ amekuwa staa, kitendo cha kumpiga Muingereza tena bondia namba nane wa dunia sio jambo dogo, hiyo ni nembo yetu kwenye ngumi,” alisema Mwamakula.

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT), Chris Mutta alisema Mwakinyo anatakiwa kupata kocha bora atakayempa mbinu za kiufundi.

“Alicheza vizuri nilichokiona alicheza kwa kasi sana kama angekutana na bondia anayemudu hadi raundi ya saba, kwa kasi aliyoanza nayo kuna uwezekano naye angechoka. Nashauri afanye mazoezi makali ya pumzi kujiandaa na pambano la Ujerumani,” alisema.