Neville, Redknapp wamtolea uvivu Pogba

Muktasari:

  • Paul Pogba amemlaumu beki wa kati ya Manchester United, Victor Linderlof kuhusika na sare ya mabao 2-2 iliyopata timu hiyo dhidi ya Chelsea kwenye uwanja wa Stamford Bridge.Pogba amemlaumu beki huyo kutokuwa makini kwenye safu ya ulinzi na kupelekea kupata sare hiyo huku wachambuzi wa soka nao wakimtaja nyota huyo wa Ufaransa kuhusika na matokeo hayo.

Manchester United imeshindwa kurejesha furaha kwa mashabiki wake, lakini Paul Pogba, amemtaja beki wa kati Victor Linderlof kuhusika na matokeo ya juzi usiku.

Man United ikiwa katika nafasi nzuri ya kupata ushindi dhidi ya Chelsea, iliduwazwa baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 ugenini kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Pogba amemlaumu Linderlof kutokuwa makini katika safu ya ulinzi, lakini wachambuzi wamemtaja nyota huyo wa Ufaransa kuhusika na kipigo hicho.

Beki nguli wa zamani wa Man United na England, Gary Neville, amemtaja Poga ndiye chanzo cha timu hiyo kupata sare.

Pia mchambuzi mwingine Jamie Redknapp alisema Pogba amechangia Man United kutopata pointi tatu katika mchezo huo.

Wachambuzi hao waliowahi kuwika katika medani ya soka walisema Pogba ‘alisinzia’ kumbana Antonio Rudger kufunga bao la kwanza.

Pogba alishindwa kumdhibiti Rudger kufunga bao la kwanza katika mchezo huo uliokuwa na ubabe mwingi baina ya wachezaji. Rudger alipiga mpira wa kichwa akiwa peke yake licha ya Pogba kuwa jirani naye.

“Ukimuangalia Pogba utamuona alikuwa amesinzia, analalamika nini wakati alikuwa katika eneo la kuzuia asifunge bao,” alisema Neville.

Redknapp alisema Pogba anastahili kubeba lawama kwa Man United kwa kutokuwa makini katika eneo la ulinzi.

Awali, Pogba alidai wachezaji wa Man United walikosa nidhamu ya mchezo na kusababisha kuambulia pointi moja.

Katika mechi nyingine zilizochezwa Ulaya mwishoni mwa wiki, Tottenham Hotspurs ilishinda bao 1-0 dhidi ya West Ham United.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City ilipata ushindi mnono wa mabao 5-0 ilipomenyana na Burnley.

Juventus ililazimishwa sare ya bao 1-1 ilipovaana na Genoa ikiwa nyumbani, Monaco ilikiona cha moto baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Strasbourg.