Rekodi yambeba Kessy kimataifa

Muktasari:

  • Nkana Red Devils ya Zambia ina beki wa Tanzania, Hassani Kessy aliyesajiliwa kutoka Yanga.

Dar es Salaam. Nuksi ya matokeo mazuri wanayopata wachezaji wa Tanzania wanaocheza soka nje ya nchi inapaswa kumalizwa na Simba itakapovaana na Nkana Red Devils ya Zambia, katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Desemba 14 hadi 16.

Nkana ina beki wa Tanzania, Hassani Kessy aliyesajiliwa kutoka Yanga.

Simba na Nkana zinakutana katika mechi za raundi ya kwanza baada ya kupenya ile ya awali. Mshindi atapata nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, wakati timu itakayotolewa itacheza hatua ya mwisho ya mtoano kusaka nafasi ya kucheza makundi ya Kombe la Shirikisho.

Rekodi ya timu za Tanzania inaonyesha huwa zinashindwa kufua dafu zinapocheza na timu kutoka nje ya nchi ambazo vikosi vyao vinaundwa na wachezaji kutoka hapa nchini.

Nyota wa Tanzania wanaocheza soka la kulipwa katika klabu za nje, wamekuwa na bahati kwa kuwa timu zao zimekuwa zikipata matokeo mazuri zinapocheza na zile za hapa kwenye mashindano mbalimbali.

Nuksi hiyo ya wachezaji wa Tanzania kuziumiza za hapa zinapokutana, zilianzia Februari 2003 wakati kiungo Shabani Kisiga alipoiongoza Sports Club Villa ya Uganda kuimaliza Simba kwenye fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup).

Kisiga, aliyekuwa kijana mdogo kipindi hicho na muda mfupi, baada ya kuingia akitokea benchi, alibadili upepo wa mechi ambayo kwa kiasi kikubwa ilitawaliwa na Simba.

Kiungo huyo mshambuliaji ambaye baadaye alisajiliwa na Simba ndiye aliyepiga pasi iliyozaa bao lililoipa ubingwa Villa. bao hilo lilifungwa na Vincent Tendwa.

Mwaka 2016 nuksi hiyo iliikumba Yanga dhidi ya TP Mazembe Englebert ya DR Congo ambayo kwenye kikosi chake ilikuwa na Mtanzania, Thomas Ulimwengu.

Ikiwa na Ulimwengu, TP Mazembe iliifunga Yanga mara mbili kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ya kwanza hapa Dar es Salaam, Yanga ilifungwa bao 1-0 kabla ya kufungwa mabao 3-1 ugenini.

Akizungumzia kitendo cha kukutana na Simba ambayo aliwahi kuitumikia, Kessy alisema yupo tayari kukabiliana na timu yake ya zamani na ataweka utanzania pembeni.

Simba ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1, dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland. Awali Simba ilishinda kwa mabao 4-1 jijini Dar es Salaam kabla ya kuilaza 4-0 ugenini.

Nkana ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 dhidi ya UD Song ya Msumbiji. Awali ilishinda ugenini kwa mabao 2-1 na baadaye kuibuka na ushindi mdogo wa bao 1-0 nyumbani.