Rooney amtaja Pep Guardiola

Mshambuliaji nguli DC United ya Marekani, Wayne Rooney,

Muktasari:

Rooney alisema timu hizo zitachuana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kuwa zote zina timu bora.

Washington, Marekani. Mshambuliaji nguli DC United ya Marekani, Wayne Rooney, amesema msimu ujao utakuwa na ushindani mkali baina ya Manchester United na Manchester City.

Rooney alisema timu hizo zitachuana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England kwa kuwa zote zina timu bora.

Rooney (32), aliyefunga mabao 253 katika mechi 491 za Ligi Kuu akiwa Everton na Man United alisema makocha wa timu hizo akiwemo Pep Guardiola wametengeza timu imara za ushindani.

Alisema Man United inayonolewa na Jose Mourinho ipo vizuri na itatoa upinzani mkali kuliko timu nyingine dhidi ya Man City katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England.

Makocha hao wamekuwa na upinzani mkali baada ya kuzinoa timu za Ligi Kuu na msimu uliopita walinogesha mashindano kutokana na tambo za mara kwa mara kila mmoja akitamba ni bora zaidi ya mwingine.

Guardiola na Mourinho waliwahi kufundi soka Hispania na mara kwa mara waliibua msuguano ndani ya uwanja wakati timu zao zikicheza.

Wakati Guardiola alikuwa akiinoa Barcelona, Mourinho alikuwa kocha watani wao wa jadi Real Madrid.

“Bila shaka msimu ujao Manchester City haitapata ubingwa k kwa urahisi, nadhani watapata ushindani kutoka timu nyingine hasa wapinzani wao wakubwa Manchester United,” alisema Rooney.

Rooney alisema ingawa Man City imekiongezea nguvu kikosi chake kwa kufanya usajili makini, lakini isitarajie mteremko katika mashindano hayo.

“Nimewasikia baadhi ya watu wakisema Man City wanacheza soka la kuvutia na kufunga mabao mengi, lakini msimu ujao hawatapata ubingwa kwa urahisi najua ugumu na ushindani unavyokuwa katika Ligi Kuu,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Man United na timu ya Taifa ya England aliyecheza kwa mafanikio Old Trafford.