Serengeti Boys bado kidogo tu

Muktasari:

Kocha Milambo aliyeiongoza Serengeti Boys kutwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri usiozidi miaka 17 hivi karibuni, aliliambia gazeti kuwa hatua ya kwanza ya maandalizi yao imekamilika.

Dar es Salaam. Kikosi cha Serengeti Boys kimeingia hatua ya pili ya maandalizi kuelekea kwenye fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) huku kocha wa timu hiyo, Oscar Milambo akianza kupiga hesabu ya kulibakisha kombe hilo nchini.

Kocha Milambo aliyeiongoza Serengeti Boys kutwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana wenye umri usiozidi miaka 17 hivi karibuni, aliliambia gazeti kuwa hatua ya kwanza ya maandalizi yao imekamilika.

“Tumeingia hatua ya pili ya maandalizi ambapo sasa tuko kwenye programu ya kuwapa vijana mbinu, tulianza na ufundi zoezi ambalo vijana wamelifanya kikamilifu na hatua tuliyopo ni ya mazoezi ya mbinu.

“Tunaamini kwa maandalizi yetu na mipango tuliyonayo bila shaka vijana watafanya vizuri na kubakisha kombe hilo nyumbani,” alisema kocha huyo.

Alisema ndoto ya vijana hao ni kuwa wachezaji wa kimataifa na anaamini kwa hatua wanayoelekea ndoto zao zitatimia.

“Ni vijana wadogo, wote wanaelekea miaka 16 sasa na bado wana muda mrefu wa kucheza soka kwani tuliichukua timu hii kwa ajili ya Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini. Licha ya umri wao mdogo lakini vijana wana morali ya kufika mbali,” alisema.

Timu hiyo inaendelea na mazoezi ya wazi kwenye Uwanja wa Karume jijini hadi Mei 20 ambapo baada ya hapo itakwenda Sweden.