Simba Day yamshtua Mbelgiji wa Simba

Muktasari:

  • Baada ya mchezo ule, kocha huyo aliwasifu wachezaji wake kwa mchezo mzuri, akakataa kumlaumu Adam Salamba kwa kukosa penalti, lakini akagoma kukubali kiwango cha washambuliaji wake akisema kuna kazi ya kufanya.

Dar es Salaam. Mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba wameishangilia timu yao kwa sare ya 1-1 dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana, lakini kocha wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems ametikisa kichwa, akasema bado kabisa.

Baada ya mchezo ule, kocha huyo aliwasifu wachezaji wake kwa mchezo mzuri, akakataa kumlaumu Adam Salamba kwa kukosa penalti, lakini akagoma kukubali kiwango cha washambuliaji wake akisema kuna kazi ya kufanya.

Katika mahojiano mafupi na Mwananchi, tathmini yake ya mchezo hasa safu ya ushambuliaji, kocha huyo alisema safu yake ya ushambuliaji kwa ujumla imemshtua.

Alisema wana kazi ya ziada ya kufanya kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwani wachezaji hawatakiwi kulionea goli aibu.

“Mechi hii ya Kotoko kutoka Ghana imenipa somo na imenishtua nini natakiwa kukifanya sasa na wenzangu.

“Tulitengeneza nafasi za kutosha lakini tulishindwa kuzitumia kwa hiyo inatakiwa kuwapa utaalamu zaidi washambuliaji wangu ili wawe makini na nafasi watakazokuwa wanatengenezewa,” alisema kocha huyo anayeiongoza Simba mjini Lindi kucheza na Mamungo ikiwa ni shamrashamra za ufunguzi wa Uwanja wa Majaliwa.

Simba ambao walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Asante Kotoko katika tamasha lao, ilitanguliwa kufungwa bao kabla ya Emmanuel Okwi kusawazisha bao hilo huku Adam Salamba akikosa penalti dakika ya 84.

Washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, Adam Salamba, Meddie Kagere walishindwa kufunga licha ya kutengenezewa mipira mingi na Cletus Chama, mchezaji kutoka Zambia aliyejizolea umaarufu katika mchezo huo.

Mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara watauanza rasmi msimu wa Ligi Kuu Bara kwa kucheza na Tanzania Prisons, Agosti 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kutetea ubingwa huo, Simba wataufungua msimu huo wa 2018/19 kwa kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Mtibwa Sugar, Agosti 18 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Simba iko mkoani Lindi na baada ya hapo itakwenda Arusha kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kwenda Mwanza tayari kwa mchezo huo wa kukata utepe.