Simba ina dakika 90 nyingine

Muktasari:

  • Mtibwa Sugar nayo imepoteza kwa kufungwa mabao 3-0 lakini zote zina dakika nyingine 90 za kuingia makundi.

Kitwe, Zambia. Wahenga walisema kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi, Simba na Mtibwa Sugar zimepoteza michezo yao ugenini jana lakini bado zina dakika nyingine 90 kwenye Uwanja wa Taifa kuonyesha kuwa wamejipanga kwa michuano hiyo.

Mabingwa hao wa Tanzania jana walikuwa kwenye Uwanja wa Nkana ikiwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kulala kwa mabao 2-1, na marudiano yake yatafanyika Desemba 22 huku Mtibwa ikichapwa 3-0 na KCCA katika Kombe la Shirikisho.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa inahitaji ushindi wa bao 1-0 au zaidi ili ifuzu hatua ya makundi wakati Mtibwa yenye mlima mrefu kuupanda, inatakiwa kushinda mabao 4-0.

Pamoja na kufungwa, wengi wa mashabiki wa Simha wanaonekana kupata ahueni kwa bao la penalti la John Bocco ambalo linaipa Simba thamani kwa kuipunguzia mzigo wa mabao.

Mchezo wenyewe

Simba ikicheza soka la kushambulia tangu mwanzo, iliwapa jeuri mashabiki wao walijitokeza uwanjani hapo kuishangilia timu yao wakitambia rekodi ya mechi zao za nyumbani.

Bao la mkwaju wa penalti uliopigwa na Bocco, uliwapa afueni ya kutosha Simba kwa mechi yao ya marudiano itakayopigwa wiki ijayo huku mashabiki wakiamini kabisa Wazambia hao hawatatoka salama jijini Dar es Salaam.

Pamoja na hayo, rekodi zinaonyesha Simba haijawahi kufungwa na Nkana katika mechi walizokutana nao jijini Dar, kwani mwaka 1994 katika hatua ya robo fainali Wekundu waliwafumua Wazambia hao kwa mabao 2-0 baada ya kulala ugenini 4-1.

Pia walikaribishwa tena kwa kipigo cha mabao 3-0 katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2002, siku chache baada ya Simba kulala ugenini kwa mabao 4-0.

Hivyo kwa kipigo cha jana, kimewapa afueni makocha, viongozi na hata mashabiki kwa kuamini kuwa mchezo ujao watamaliza kazi mapema na timu kutinga makundi kwa mara ya pili tangu michuano hiyo ibadilishe mfumo wake.

Katika pambano hilo, mabeki wa Simba waliokuwa chini ya Pascal Wawa, Erasto Nyoni Nkana na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ walikuwa wakifanya makosa, huku kipa Aishi Manula akiendelea kufungwa mabao ya mashuti ya mbali.

Wenyeji walitawala kipindi cha kwanza kwa kuonyesha kiu ya kutaka ushindi nyumbani na beki Hassan Kessy aliyewahi kuzichezea Simba na Yanga alipiga krosi iliyokutana na Ronald Kampamba aliyepiga kichwa kilichogonga mwamba na kuokolewa na mabeki wa Simba.

Ndani ya dakika 16 Nkana walikuwa wakiutawala mchezo kwa kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza huku mbinu za Simba zikionekana kugonga mwamba kupenya katika safu ya ulinzi ya Nkana.

Simba ilishtuka dakika 17 walipata faulo ambayo ilikuwa shambulio la kwanza baada ya mshambuliaji, Emmanuel Okwi kupiga faulo ambayo ilitaka kuzaa bao hata hivyo kipa Allan Chibwe aliupangua mpira.

Shambulizi hilo liliwashtua Nkana kwani waliongeza spidi ya kushambulia na dakika 27 Ronald Kampamba alifungia bao kali la kuongoza kwa kumchungulia kipa Aishi Manula na kuukwamisha mpira kimiani.

Kipindi cha pili Simba walianza kwa umakini zaidi kwa kupigiana pasi za haraka haraka huku wakilisogelea lango la Nkana, mbinu ambayo ilionekana kuwa na tija kwani dakika 47 James Kotei alipiga shuti kali hata hivyo kipa wa Nkana, Allan Chibwe aliudaka mpira huo kwa umakini.

Nkana walikuwa wanapanga mashambulizi yao kwa umakini na dakika 56 Kelvin Kampamba aliiongezea Nkana bao la pili baada ya kuwatoka mabeki wa Simba na kupiga shuti lililomshinda Aishi Manula pembeni kushoto kwake.

Simba ilifanya mabadiliko dakika 61 kwa kumtoa Emmanuel Okwi na kumuingiza Shiza Kichuya aliyeiongezea nguvu timu hiyo bao la penalti dakika ya 73 baada ya Meddie Kagere kuchezwa rafu na Mussa Mohammed na Bocco alitumbukiza wavuni mkwaju wake kiufundi na kufufua matumaini ya Msimbazi.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema bao walilopata ugenini ni mtaji wa kumaliza kazi katika mechi ijayo, licha ya kukiri vijana wao walishindwa kucheza vile alivyotaka.