Simba wana uhakika na Kombe la Kagame

Muktasari:

  • Simba ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliomalizika na huo ni wa 19 tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1965.

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Masoud Djuma amefunguka na kusema, kikosi chao kitafanya vizuri katika Mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii.

Djuma amesema, sababu kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo hata kama watakutana na timu zilizomfunga kwenye mashindano ya Kombe la Sportpesa yaliyofanyika Kenya kwa sababu wamejiandaa vizuri na wana kila kitu.

 "Sasa hivi tupo nyumbani tuna kila sababu ya kufanya vizuri tofauti na ilivyokuwa Kenya, tuna wachezaji wazuri na wana morali ya juu," alisema Djuma.

Masoud ameongeza kwa kusema, wameamua kuanza mazoezi mapema ili kupata nafasi ya kuangalia baadhi ya wachezaji wapya na ambao wamemaliza mikataba kama wanaweza kuwaongeza mipya.

"Huwezi ukasema mchezaji hana kiwango wakati alikuwa hapati nafasi ya kucheza, sasa hivi ni muda sahihi wa kuangalia wachezaji vizuri kabla ya kuachana nao, pia kuwaangalia vizuri wale wapya kabla hatujawasainisha," Djuma alisisitiza.