#WC2018: TUJIKUMBUSHE: Historia kujirudia Ufaransa vs Croatia?

Muktasari:

  • Wakati mashabiki ulimwengu mzima wakijiandaa kushuhudia mechi ya kukata na shoka kati ya Ufaransa na Croatia, ni kwamba Ubelgiji ndio washindi wa tatu wa michuano hii. Mabao ya Thomas Muenier na nahodha Eden Hazard yalitosha kuwazima wajukuu wa Malkia na wimbo wao wa 'Its coming home'

Moscow, Russia. Hatimaye ile fainali iliyosubiriwa kwa hamu, ndio ishafika hiyo mwanangu. Tunahesabu masaa tu kabla Uwanja wa Luzhniki haujaandika historia nyingine ya michuano ya Kombe la Dunia. Hii itakuwa zaidi ya fainali, sijui itakuwaje lakini mbona patachimbika tu.

Wakati mashabiki ulimwengu mzima wakijiandaa kushuhudia mechi ya kukata na shoka kati ya Ufaransa na Croatia, ni kwamba Ubelgiji ndio washindi wa tatu wa michuano hii. Mabao ya Thomas Muenier na nahodha Eden Hazard yalitosha kuwazima wajukuu wa Malkia na wimbo wao wa 'Its coming home'

 

 

Kabla ya kuelekea Moscow uliko uwanja wa Luzhniki, wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 81,000, Mwanaspoti ambayo imekuwa na kazi ya kukujuza na kukuhabarisha kuhusu matukio yote yanayojiri nchini Russia bila kusahau takwimu na kumbukumbu muhimu ya michuano hii, inakurudisha miaka 20 iliyopita.

Mwaka 1998, katika mechi ya nusu fainali, Croatia ikiongozwa na mfungaji bora wa mwaka huo, Davor Suker, waliingia dimbani kupambana na wenyeji ufaransa baada ya kuilima Ujerumani iliyokuwa inapigiwa upatu kushinda taji hilo, 3-0 katika hatua ya robo fainali.

 

 

Kwa wasiojuwa, mechi ile ya nusu fainali ina chembechembe za kufanana na mechi ya leo. Katika fainali za mwaka huu Les Blues wameonesha kiwango kizuri wakianza na kuitandika Argentina ya Lionel Messi 3-0 katika hatua za makundi, wakiwa na beki bora kabisa.

Kabla ya kukutana na Croatia mwaka ule, France wakiwa na wachezaji nyota kama Zinedine Zidane na Thiery Henry, wakimaliza hatua ya makundi katika kiwango bora kabisa ambapo waliruhusu kufungwa bao moja tu. Ikumbukwe pia kwamba katika mechi ile, Didier Deschamps alikuwa nahodha na sasa ndiye Kocha wa Les Blues.

Kipindi cha kwanza cha mechi ile, ilimalizika kwa sare tasa. Michuano ya mwaka huu, tumeshuhudia mechi nyingi zikiisha kwa sare tasa katika kipindi cha kwanza, ushindi ukipatikana kipindi cha pili. Kama ilivyokuwa mwaka ule Ufaransa wakaibuka kwa ushindi wa 2-1.

Kombe la dunia mwaka huu, mechi 22, zilieenda mapumziko zikiwa sare tasa. Kiujumla mabao 61 tu ndio yaliyofungwa katika kipindi cha kwanza huku 97 zikiwekwa kambani kipindi cha pili. Sio utabiri lakini kama ilivyokuwa mwaka 1998, mechi inaweza ikamalizika kwa ushindi mwembamba wa 2-1 au 1-0.

Usiku ule, baada ya kwenda mapumziko wakiwa sare 0-0, Croatia waliingia na nguvu mpya wakipata bao la mapema katika kipindi cha pili kupitia kwa Davor Suker, aliyeweka kambani bao lake la sita kwenye michuano ile. Watoto wa Mama wakawa na uhakika wa kusonga mbele, wakaanza kushangilia mapema, wakajisahau.

 

 

Kama ilivyokuwa mwaka huu, ambapo ushindi wa Ufaransa ulitokana na kazi ya Mwafrika Samuel Umtiti, ambaye ni beki, ndivyo usiku ule Les Blues walivyohitaji miguu meusi ya Lilian Thuram kutoka salama. Thuram mweusi kama alivyo, mgumu kama alivyo na roho yake ngumu, akatupia wavuni  mara mbili na kuimaliza Croatia. Safari yao ikaishia hapo!

Ni kama usiku wa 1998 unaeza kujirudia pale Luzhniki. Sio utabiri wala ramli, lakini kuelekea mechi ya leo, mashabiki wa Croatia na Ufaransa wajiandae kisaikolojia maana lolote linaweza kutokea.

Salamu zangu kwa Mama Kolinda Grabar-Kitarović, Davor Suker na Didier Deschamps, wasitegemee mabao mengi maana takwimu za mwaka huu, zinaonesha kuwa mechi 14 zilimalizika kwa ushindi wa 2-1 huku 15 zikimalizika kwa ushindi wa  1-0. Asanteni kwa kuja. Tukutane Luzhniki wajomba!