Yanga SC yaanza mambo, yampiga mtu mkono

Muktasari:

  • Hata hivyo, kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera alisema anataka mechi ngumu za kirafiki ili kupima wachezaji.

Morogoro. Timu ya Yanga imecheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya timu ya kituo cha soka cha Tanzanite na kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 mjini hapa.

Hata hivyo, kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera alisema anataka mechi ngumu za kirafiki ili kupima wachezaji.

Katika mchezo huo wa jana ambao Zahera alichezesha vikosi viwili tofauti kwa kila dakika 45, Yanga ilionekana kuelewana zaidi dakika 45 za kwanza.

Ikicheza soka la kasi Yanga ilimaliza dakika 45 za kwanza ikiongoza kwa mabao 4-1 yaliyofungwa na Heritier Makambo, Mrisho Ngassa na viungo Deus Kaseke, Emmaneul Martin na Pius Buswita wakati bao la Tanzanite likifungwa na Omari Jaribu.

Zahera aliwaanzisha kipa Benno Kakolanya na mabeki Juma Abdul, Mwinyi Haji, Andrew Vincent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja.

Katika kiungo kikosi hicho kilichotengeneza sehemu kubwa ya ushindi huo kilikuwa na nyota Feisal Salum ‘Fey Toto’, Buswita, Raphael Daud, Ngassa, Kaseke huku mshambuliaji akiwa Makambo.

Kipindi cha pili Zahera alibadili kikosi kizima ambacho licha ya kupoteza nafasi nyingi, kilitengeneza bao moja pekee likifungwa na Martin aliyepata pasi ya kiungo Edward Maka.

Kikosi hicho kilikuwa na nyota Klause Kindoki, Juma Mahadhi, Gadiel Michael, Pato Ngonyani, viungo wakiwa Thabani Kamusoko, Jafari Mohammed aliyetolewa na kungia Maka, Said Juma, Yusuf Mhilu aliyetolewa na kuingia Martin wakati washambuliaji ni Amissi Tambwe na Matheo Antony.

Akizungumzia mechi hiyo Zahera alisema amepata kipimo kizuri kwa wachezaji wake, lakini ameomba kutafutiwa mechi ngumu kupima ubora wa wachezaji wake.

Zahera alisema endapo atapata mechi mbili na vikosi vigumu atajua ubora wa timu yake kabla ya kukutana na USM Alger ya Algeria katika mechi ya Kombe la Shirikisho.

“Hii ni mechi ya kwanza lakini sitaki kuzingatia chochote kilichotokea leo (jana) bado nahitaji mechi ngumu kama mbili kabla ya kukutana na USM Alger,” alisema Zahera.