Yanga yasaka pointi kwa Ruvu Shooting

Muktasari:

  • Ligi Kuu Bara Tanzania Bara michezo inaendelea leo kati  ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ni kama unawachongisha washambuliaji hatari wa timu hizo mbili, Heritier Makambo na Said Dilunga wenye mabao nane

Dar es Salaam. Mchezo wa leo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ni kama unawachongisha washambuliaji hatari wa timu hizo mbili, Heritier Makambo na Said Dilunga wenye mabao nane kila mmoja.

Washambuliaji hao wa kutegemewa kwenye klabu hizo, watakutana pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku kila mmoja akiwa na jeshi lake kupigania pointi tatu muhimu za mchezo huo.

Mabao ya Makambo yamechangia kwa kiasi kikubwa Yanga kuwa vinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, wakiwa na pointi 41, walizozikusanya kwenye michezo 15.

Dilunga kwa upande wake amechangia kuifanya Ruvu Shooting kutoka Pwani, kuvuna pointi 17 kwenye michezo 16, wazee hao wa kupapasa wana wastani wa kupata alama moja kwenye kila mchezo.

Rekodi zaibeba Yanga

Yanga inayosaka pointi kwa udi kujiimarisha kileleni, inabebwa na rekodi kwani ndani ya misimu miwili iliyopita 2016/17 na 2017/8, Yanga inaonekana kuwa na rekodi nzuri mbele ya Ruvu Shooting.

Katika michezo minne ambayo wamekutana kwenye Ligi, Yanga imeibuka na ushindi mara tatu huku Ruvu Shooting wakiambulia sare mara moja kwenye mchezo wa mwisho kukutana, Mei 25 mwaka huu ya mabao 2-2.

Michezo wa kwanza, Yanga kuifunga Ruvu ndani ya misimu miwili iliyopita ilikuwa Novemba 10, 2016 kwa mabao 2-1 na baadaye wakashinda mzunguko wa pili, Machi Mosi mwaka jana kwa mabao 2-0.

Kabla ya sare ya mabao 2-2 ambayo msimu uliopita kwenye mchezo wao wa mwisho kukutana, Yanga waliishushia kipigo Ruvu kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza cha bao 1-0, Januari 21.

Makocha watambiana

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema maandalizi ya kikosi chake yamekwenda vizuri japo kuna baadhi ya wachezaji watakosekana kwenye mchezo huo ila atahakikisha wanapata pointi tatu.

“Feisal Salum ‘Fei toto’ alipata msiba kwa hiyo alienda mara moja kwao Zanzibar, Kelvin Yondani ana kadi tatu za njano, Mrisho Ngassa ataendelea kutumikia adhabu ya kadi nyekundu na Raphael Daud aliumia kwenye mechi dhidi ya Biashara United,” alisema Zahera.

Upande wake kocha wa Ruvu Shooting, Abdulmutik Haji alisema pamoja ya kuwa Yanga ni timu kubwa wataingia na mbinu za kuishambulia huku wakijilinda kwa umakini.

KMC vs Prisons

Mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Uhuru, KMC iliichakaza Prisons ya Mbeya mabao 4-1, mchezo uliokuwa wa ushindani.