Zahera aichongea Simba

Muktasari:

  • Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema kitendo cha wapinzani wao kukaa wiki mbili bila kucheza mchezo wa ligi, kinatoa tafsiri mbaya katika maendeleo ya soka nchini.

Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imesema kuna mchezo mchafu unafanywa dhidi yao ili kuwadhoofisha katika mbio za ubingwa wa soka wa Tanzania Bara.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alidai jana kuwa ratiba ya Ligi Kuu inaibana timu yake na kutoa nafasi kwa Simba ambao ni watanio wao wa jadi.

Zahera alisema kitendo cha wapinzani wao kukaa wiki mbili bila kucheza mchezo wa ligi, kinatoa tafsiri mbaya katika maendeleo ya soka nchini.

Yanga, ambayo inashika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ikiwa na pointi 38, imecheza mechi 14 huku vinara Azam wakiwa na pointi 39 baada ya kucheza mechi 15. Simba, ambayo inashiriki raundi za awali za Ligi ya Mabingwa wa Afrika, imecheza mechi 12.

Leo Yanga inavaana na Biashara United, katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa na itacheza dhidi ya Kinondoni FC, Coastal Union na Singida United ifikapo Desemba 30.

“Haiwezekani timu nyingine ziwe zimecheza mechi mfululizo na nyingine zikiwa na viporo, hiyo inapunguza ubora na ushindani kwenye ligi,” alisema kocha huyo Mcongo.

“Nilizungumza na wachezaji wangu kuhusu ratiba ya ligi inavyotubana. Tunacheza mechi nne kwa siku 12. Viongozi wanaosimamia mpira wanasababisha usipande, hauwezi kuendelea wakati mnakuja na malengo kwamba timu fulani ndio inapaswa kubeba kombe.”

Kocha huyo alisema ligi ambayo imekuwa ikiwachosha wachezaji wake na kutoa fursa kwa Simba kucheza kwa ufanisi.

Hata hivyo, kocha huyo alisema hana hofu na timu zinazoshiriki ligi hiyo kwa kuwa ana kikosi imara, lakini wasiwasi wake ni viongozi wa ligi kukosa uaminifu.

“Yanga tulicheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita. Tulitoka Kenya siku ya pili tukaenda Shinyanga kucheza mechi ya ligi, siku ya tatu unakwenda Mbeya unatoka Mbeya unakwenda Rwanda unarudi unakwenda Songea,” alisema.

“Simba imecheza juzi Ligi ya Mabingwa Afrika, ligi atacheza siku gani? Hata Barcelona wanacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na baada ya siku tatu wanacheza ligi kwa sababu wanasimamia soka kwa utaratibu.”

Maoni yake yameungwa mkono na nyota wa zamani wa Taifa, Mohamed Rishard “Adolph”.

“Zahera ameongea ukweli mtupu. Namuunga mkono kila alichosema. Ligi yetu inaongozwa kimipango ndiyo maana haina ushindani,” alisema Adolph.

“Kuanzia upangaji wa ratiba na waamuzi ndiyo janga kabisa. Yaani wanafanya watu wahamie kutazama ligi za Ulaya. Ni aibu kubwa hadi kocha mgeni kaamua kusema.”

Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema wamesikia kilio cha Zahera na wamechukua ushauri wake na watafanyia kazi.

“Tumesikia tutachukua ushauri wake na kuufanya kazi, hakuna kitakachoharibika hapo,” alisema Wambura.