Zahera apangia mabao washambuliaji wake

Muktasari:

  • Kocha huyo amesema lazima kuwa na malengo ya kufunga na kuwataka washambuliaji kila mmoja kuwa na mabao yake ya kufunga yatakayoibeba timu hiyo.

Morogoro. Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amewapangia mafowadi wake mabao ya kufunga Ligi Kuu huku akipunguza dozi ya mazoezi kwa wachezaji wake akibadili ratiba ya mazoezi.

Kocha huyo amesema lazima kuwa na malengo ya kufunga na kuwataka washambuliaji kila mmoja kuwa na mabao yake ya kufunga yatakayoibeba timu hiyo.

“Hata ucheze mpira mkubwa kiasi gani, bila mabao hujafanya kitu, nguvu yangu ninaielekeza huku.” Yanga ambayo bado imeweka kambi hapa Mkoani Morogoro ikifanya mazoezi katika Uwanja wa Highland Park imekuwa na ratiba kali ya mazoezi.

Tangu kikosi hicho kifike hapa wiki moja sasa ratiba kamili ya mazoezi ilikuwa ni kufanya mara mbili kwa siku. Kocha Zahera amekuwa akiwapeleka vijana wake mazoezini asubuhi wakitumia saa tatu na kurudi tena jioni saa 10.

Juzi na jana Zahera aliwapumzisha wachezaji ikiwa ni mara ya kwanza tangu wafike hapa akiwaambia wakusanye nguvu kwa ajili ya jioni ya jioni.

Ratiba hiyo ya juzi na jana ilikuwa maalumu kwa mazoezi ya mbinu kazi ambayo alianza nayo juzi katika mazoezi yake.

Kocha Zahera alisema kwasasa anaona mambo yanaenda sawa kwa wachezaji wake kuimarika ambapo wamemaliza wiki mbili za mazoezi makali ya kujaza pumzi na stamina.

Alisema bado waana kazi kubwa ya kufanya kumalizia kuijenga timu hiyo ingawa kwasasa watakuwa wakielekeza nguvu kubwa kufanya mazoezi ya mbinu.

“Nimewapumzisha kidogo leo (jana) tumekuwa na wiki moja ya mazoezi makali sana kidogo naona vijana wanakuwa sawa kama tunavyotaka,”alisema Zahera.

“Tuna ratiba ya mazoezi tunayotaka sasa ni vyema tukawapa nafasi ya kupumzika wametumika kwa nguvu kubwa.”