Simba, Yanga zimebeba taswira ya Tanzania

Muktasari:

  • Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe anasema Simba na Yanga, zinaenda kuwakilisha taifa, hivyo utani wa jadi baina yao, usihusike kimataifa.

SIMBA ikisafiri kuwafuata Djibouti kucheza na wenyeji wao Gendarmerie, huku Yanga wamekwenda Shelisheli, kucheza na St Louis, zimekumbushwa kuvaa utaifa na kujua Watanzania wapo nyuma yao.

Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe anasema Simba na Yanga, zinaenda kuwakilisha taifa, hivyo utani wa jadi baina yao, usihusike kimataifa kwa kuwataka wachezaji wa klabu hizo watangulize utaifa.

"Tushindane kwa ligi ya ndani,tunapocheza na mataifa mengine, tubadilike kuanzia wachezaji hadi mashabiki kuziombea na kuziunga mkono, ili hata wakija kucheza uwanja wa nyumbani wasipate mpenyo wa kushinda,"anasema.

 

Staa wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua anasema neno utaifa likifanyia kazi kwa Watanzania ndipo hatua katika soka zitapatikana akisisitiza kwamba hakuna haja kuweka utofauti wakati hizo klabu zinawajibika kuwakilisha nchi.

"Upinzani wa ndani usiingilie pale Simba na Yanga,zinaposhiriki michuano ya kimataifa,tuziombee kwa pamoja ili ziweze kupeperusha bendera ya taifa vema kama vile tunavyowaombea watu wa riadha,"anasema.