Washambuliaji Simba utulivu bado

Muktasari:

  • Kiungo huyo aliwaho kucheza Simba kabla ya kutimkia Norway alipokuwa akicheza soka la kulipwa

Dar es Salaam. Kiungo wa Mtibwa Sugar, Henry Joseph 'Shindika' amewataka washambuliaji wa Simba kutuliza akili wanapofika ndani ya 18, ili iwasaidie timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika yatakayoanza mwakani.

Nahodha huyo wa zamani wa Simba, Shindika alisema amegundua tatizo hilo baada ya timu yake ya Mtibwa kupata sare 1-1 na Simba, hivi karibuni Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

"Simba ipo vizuri, labda safu ya ushambuliaji inakosa sana mabao, hilo linatokana na kukosa utulivu, nawashauri kuelekea mashindano yao ya kimataifa wajitahidi kutuliza akili zao itawasaidia na wanaweza kufika mbali."

"Timu inayoshiriki mashindano ya kimataifa, inasimama kuwakilisha nchi yake ndiyo maana klabu kongwe ambazo ndizo zenye tiketi lazima zitulize akili zicheze kitaaluma mbele ya mataifa mengine."

Kiungo huyo alimsifu mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi kuwa bado ana kasi nzuri.

"Anaonyesha uwezo wake binafsi hii inamsaidia kujitofautisha na chipukizi, kwa kweli yupo vizuri," alisema Shindika.