Xavi asema hakuna kama Iniesta

Kiungo nguli wa Barcelona,Andres Iniesta amebebwa na wachezaji wenzake wa timu hiyo wakati wa kumuaga rasmi alipocheza mchezo wa mwisho katika kikosi hicho dhidi ya Real Socirdad kwenye uwanja wa Nou Camp Hispania.Picha na AFP

Muktasari:

Kauli ya Xavi imekuja muda mfupi baada ya Iniesta juzi usiku kuaga wachezaji na mashabiki wa Barcelona katika mchezo dhidi ya Real Sociedad.

Madrid, Hispania. Kiungo nguli wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez amemtaja pacha wake, Andres Iniesta ni mchezaji wa aina yake.

Kauli ya Xavi imekuja muda mfupi baada ya Iniesta juzi usiku kuaga wachezaji na mashabiki wa Barcelona katika mchezo dhidi ya Real Sociedad.

Iniesta alibubujikwa machozi alipoaga rasmi baada ya kucheza kwa mafanikio Barcelona kwa miaka 16 katika kikosi cha kwanza.

“Huyu ni mchezaji wa aina yake kuwahi kutokea katika historia ya Hispania,” alisema Xavi aliyekuwa akicheza pacha na Iniesta katika safu ya kiungo kwa miaka 13.

Iniesta, aliyetwaa ubingwa wa Ulaya na Dunia, ana rekodi ya kuvuna mataji 32 akiwa Barcelona aliyojiunga nayo tangu akiwa kinda.

“Kwangu Andres ni mchezaji mwenye kipaji ambaye sijawahi kumuona mtu kama yeye duniani kote. Ni kiongozi uwanjani na muda wote amekuwa akitaka mpira,” alisema Xavi.

Xavi na Iniesta waliotwaa ubingwa wa Hispania mara saba na Kombe la Ulaya mara nne, walicheza kwa kiwango bora eneo la kiungo Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania.

“Kuna mtu aliniambia Xavi nimeona mchezaji mwenye kipaji katika timu ya watoto, nadhani atakufaa ana kipaji kama wewe. Alikuwa bora zaidi yangu anamiliki mpira, anatoa pasi na kucheza nafasi nyingi uwanjani,” aliandika Xavi katika barua aliyoandika wakati wa kumuaga Iniesta.

Iniesta alisema kuwa anaondoka Barcelona akiwa na majonzi baada ya kudumu kwa miaka 22 tangu akicheza shule ya watoto ya klabu hiyo.

Nguli huyo alisema moyo wake siku zote utabaki Barcelona kwa kuwa ni klabu kubwa aliyoipenda tangu akiwa kinda.

Mashabiki 90,000 juzi usiku walimuaga nyota huyo mwenye miaka 34 kwenye Uwanja wa Nou Camp.