Madaktari Brazil wamchunguza Neymar

Rio de Janeiro, Brazil. Neymar ameanza mazoezi rasmi chini ya jopo la madaktari nchini Brazil.

Mshambuliaji huyo amefanyiwa vipimo vya kina na madaktari bingwa kabla ya kujiunga na kambi ya timu ya Taifa.

Neymar alifanyishwa mazoezi mepesi ya viungo kumpima afya kabla ya kuanza mazoezi ya uwanjani.

Nahodha huyo wa Brazil, anapambana kurejea katika ubora wake kabla ya kuanza fainali za Kombe la Dunia Juni 14 nchini Russia.

Nyota huyo alikosa sehemu kubwa ya mechi za mzunguko wa pili akiwa na klabu ya Paris Saint Germain (PSG).

Neymar ameibua hofu kama anaweza fiti kucheza fainali hizo kutokana na kukaa nje ya uwanja muda mrefu akiuguza jeraha la kifundo cha mguu.

Februari, Neymar aliumia kifundo cha mguu katika mchezo walioshinda mabao 3-0 dhidi ya Marseille, baada ya kupigwa kwanja na Bouna Sarr. Wiki hii mchezaji huyo alionyesha mafanikio ambapo baadhi ya picha zilimuonyesha akiruka na hakupata maumivu.

Brazil iliyotwaa Kombe la Dunia mara tano, inatarajiwa kucheza mechi za kirafiki dhidi ya Croatia, Austria kabla ya kufungua pazia na Uswis Juni 17 na baadaye itazivaa Serbia na Costa Rica.