Panga la Mfaransa Simba kuwapitia mastaa hawa

Muktasari:

Simba inatarajiwa kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Dar es Salaam. Kocha Mfaransa Pierre Lechantre, amepanga kufumua kikosi chake na kukisuka upya kwa mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.

Katika mkakati huo, Lechantre anatarajia kuwatema wachezaji zaidi ya saba ili kutoa nafasi kwa wapya kusajiliwa.

Simba inatarajiwa kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.

Hata hivyo, Lechantre atakuwa na uhakika wa kutimiza ndoto yake endapo klabu ya Simba itamuongeza mkataba mpya.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema mkataba wa Lechantre unatarajiwa kujadiliwa na Kamati ya Utendaji baada ya kumalizika mechi za Ligi Kuu Jumatatu wiki ijayo.

Akizungumza jana, Lechantre alisema anataka kuisuka Simba iwe na nguvu ya kushindana na miamba mingine ya soka Afrika katika mashindano ya kimataifa, hivyo atalazimika kuwatema baadhi ya wachezaji maarufu.

Panga la wachezaji saba linatarajia kuwapitia Juuko Murshid, Laudit Mavugo, Juma Liuzio, Jamal Mwambeleko, Mwinyi Kazimoto, Mohammed Ibrahim na Nicholas Gyan.

Kazimoto, Mavugo na Ibrahim mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu na uwezekano wa kuongezwa ni mdogo wakati Gyan licha ya kucheza mara kwa mara anatarajiwa kutolewa kwa mkopo.

Lechantre alisema baadhi ya wachezaji hakuridhika na viwango vyao tangu alipoanza kazi Simba na ametoa baraka kutolewa kwa mkopo au kuachwa.

“Wachezaji wote ni wazuri lakini uwezo wao unazidiana, kuna baadhi ambao nitawaambia kama wamepata timu za kucheza ruksa kuondoka, wameshindwa kupata nafasi na viwango vyao vitapotea,” alisema Lechantre.

Lechantre alisema anataka washambuliaji wawili, beki wa kati na kulia, kiungo mkabaji na winga mmoja ambao watakuwa na tija katika program yake.

“Mkakati wangu kuwa na wachezaji 11 bora ambao wataanza katika kikosi cha kwanza, pia nataka watakaokuwa benchi wawe na uwezo kama walioanza kikosi cha kwanza,” alisema Lechantre.

Gharama

Msimu huu Simba ilitumia Sh1.3 bilioni katika usajili wa wachezaji 14, ambao ni Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, John Bocco, Yusuph Mlipili, Salum Mbonde, Said Mohammed, Emmanuel Mseja, Ally Shomari, Jamal Mwambeleko, Poul Bukaba na Nicholas Gyan.

Thamani ya usajili iliongezeka katika dirisha dogo, baada ya kumpata beki Mghana Asante Kwasi kutoka Lipuli na kwa ujumla wao ndio walioipa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.