Ni nusu fainali ya Simba Vs Mtibwa Uhai Cup

 LEO ndio leo katika viwanja vya Chuo Kikuu Dodoma kwani kunategemewa kutakuwa na mechi mbili kali za vijana katika Kombe la Uhai Cup.

Mechi hizo ambazo zitakuwa ni nusu fainali katika mashindano hayo, itaanzwa kuchezwa mechi Azam dhidi ya Stand United, saa saba mchana  na kisha Mtibwa dhidi ya Simba utakaopigwa saa tisa jioni.

Katika mechi hizo zote, kuna wachezaji ndio wameshika hatma ya vilabu vyao kutokana na uwezo wao wanapokuwa uwanjani, lakini vilevile uzoefu wao waliokuwa nao katika maisha ya soka.

Kwa upande wa kikosi cha Azam kilichopo chini ya kocha Meja Mstaafu Abdul Mingange, kitakuwa na nyota Paul Peter ambaye alikuwa akitumika katika kikosi cha wakubwa lakini vilevile alikuwa kama mshambuliaji tegemeo katika kikosi cha Ngorongoro Heroes (Under 20).

Katika kikosi cha Mtibwa Sugar, kinaongozwa na nyota ambaye pia ni Nahodha wa kikosi hicho pamoja na Ngorongoro Heroes, Dickson Job ambaye ni mtulivu anapokuwa yupo uwanjani.

Wachezaji hawa wote wana kila sababu ya kuzisaidia timu zao kutokana na uzoefu na utimamu wa mwili walionao baada ya kucheza mechi nyingi mfululizo wakiwa katika timu ya Vijana Taifa pamoja na klabu zao.