#WC2018 Southgate asifu kiwango cha England uwanjani

Kocha wa England, Gareth Southgate amesifu moyo wa kujituma kwa wachezaji wa kikosi chake pamoja na ushirikiano walioonyesha uwanjani na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tunisia jana Jumatatu usiku.

Mchezo huo ambao ulionekana ungemalizika kwa sare ya 1-1, Harry Kane aliongeza bao dakika za majeruhi.

Kocha huyo alisema hata kama wangeibuka na sare bao 1-1 angejivunia kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na kikosi chake.

Alisema wiki chache kabla ya mchezo huo amekuwa akizungumza mara kwa mara kuhusu umuhimu wa wachezaji kuonyesha kiwango chao na ndicho walichokifanya jana.

Kocha huyo wa England amesema timu inapocheza ka  kiwango ubora uwanjani ni rahisi kurekebisha makosa ambayo yamejitokeza.

Southgate alisema hata kama kuna mambo hawakuweza kuyarekebisha kwenye mchezo usiku wa jana, lakini walicheza vizuri.

Alisema iwapo timu Tunisia wasingepata penalti anaamini kwamba lazima tu wangeibuka na ushindi. Hata hivyo, baada ya kusawazisha matumaini ya kuibuka na ushindi yakapungua licha ya timu yake kucheza kwa kiwango cha hali ya juu.

Alimpongeza nyota wa mchezo huo Kane, huku akisema kwamba atatolea ufafanuzi zaidi kuhusu uwezo wake wa kufunga.