Arsenal mambo magumu!

London, England. ARSENE Wenger amepigwa chini, lakini bado Arsenal imeendelea kuwa wepesi pindi inapokutana na wababe wenzake wa Top Six kwenye Ligi Kuu ya England.
Imekubali tena kipigo cha mabao 3-2 mbele ya Chelsea ikiwa ni cha pili baada ya kupigwa 3-0 na Manchester City kwenye mechi ya ufunguzi iliyopigwa uwanjani Emirates.
Mashabiki waliamini kuwa Profesa Arsene Wenger ameishiwa mbinu za kupambana na makocha wenye damu change kama Pep Guardiola na Jose Mourinho, hivyo wakapambana na kuletewa Emery Unai kutoka PSG ya Ufaransa.
Hata hivyo, mambo bado ni magumu na Arsenal wamepoteza mchezo wa pili mfululizo katika Ligi Kuu ya England.
Kinachowaumiza zaidi mashabiki wa Arsenal ni kwamba, wamefungwa mechi zote na timu za Top Six ambazo zinawania ubingwa na nafasi za juu kwenye msimamo.
Katika mchezo wa jana uliopigwa kwenye dimba la Stamford Bridge jijini London, Chelsea ilianza kufungua akaunti ya mabao kupitia kwa Pedro Rodriguez katika dakika ya tisa tu kabla ya Alvaro Morata kupachika la pili dakika ya 20.
Mabao ya Chelsea yalitokana na kazi nzuri ya Willian na beki wa kushoto, Marcos Alonso ambaye alikuwa akipanda na kushuka na kusumbua ngome ya ulinzi ya Arsenal iliyoonekana kutokuwa na maelewano mazuri.
Hata hivyo, Arsenal walitulia na kutengeneza mashambulizi langoni mwa Chelsea, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kwa Pierre Aubameyang na Henrikh Mkhitaryan kushindwa kumalizia nafasi za wazi.
Lakini, makossa hayo hayakuwavunja nguvu Arsenal na dakika ya 37 Mkhitaryan alibadili matokeo na kuwa 2-1 baada ya kumalizia krosi ya Aubameyang ambayo Willian alizembea kuokoa kabla ya Alex Iwobi kuisawazishia Arsenal dakika tatu kabla ya mapumziko na matokeo kuwa 2-2.
Hata hivyo, wakati Arsenal wakiamini mchezo huo unaweza kumalizika kwa sare ya 2-2, Alonso alizamisha jahazi la Emery kwa kupachika bao la tatu na kupeleka kilio Emirates.
Kwa matokeo hayo, Chelsea inayonolewa na Maurizio Sarri ina pointi sita baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo, ambapo awali ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Huddersfield.

CHELSEA: Kepa, Azpilicueta, Rudiger, David Luiz, Alonso, Jorginho, Kante, Barkley, Willian, Pedro, Morata.
ARSENAL: Cech, Bellerin, Sokratis, Mustafi, Monreal, Guendouzi, Xhaka, Iwobi, Ozil, Mkhitaryan, Aubameyang.

MATOKEO MENGINE
Cardiff City 0-0 Newcastle United
Chelsea 3-2 Arsenal
Everton 2-1 Southampton
Leicester City 2-0 Wolves
Tottenham 3-1 Fulham
West Ham 1-2 Bournemouth2