Yanga kuosha nyota kwa USM Alger

Dar es Salaam. Pamoja na Yanga kucheza mechi mbili za kuhitimisha ratiba kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, benchi la ufundi la timu hiyo limesema litautumia mchezo wa Jumapili dhidi ya Waarabu kujenga heshima na maandalizi ya Ligi Kuu Bara.
Yanga itacheza na USM Alger ya Algeria leo Jumapili jijini Dar es Salaam, mchezo ambao una umuhimu mkubwa kwa Waarabu hao huku Yanga hata kama itashinda matokeo yake hayawezi kuifikisha popote.
Yanga inashika nafasi ya mwisho kwenye kundi lake ikiwa na pointi moja baada ya kushindwa kuzichanga karata zake katika mechi zake nne za awali za makundi kwa kukubali kipigo nyumbani na ugenini dhidi ya Gor Mahia ya Kenya. Ilifungwa mabao 4-1 kabla ya kuchapwa mabao 3-2 Dar es Salaam.
Awali ilifungwa 4-0 na USM Alger nchini Algeria na kutoka sare ya 1-1 na Rayon Sport jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, matokeo hayo hayajainyong’onyesha Yanga kuelekea kwenye mchezo huo ambao imesema itautumia kwa ajili ya kujenga heshima ya klabu yao.
“Ni kweli tumepoteza nafasi ya kusonga mbele kimataifa, lakini matokeo hayo hayo hayamaanishi tutabweteka katika mchezo wetu na Waarabu, tutapambana kuweka heshima,” alisema kocha msaidizi wa timu hiyo, Noel Mwandila.
Alisema wanaupa uzito mchezo huo ambao ni wa muhimu kwa USM Alger ambayo inasaka nafasi ya kuongoza kundi hilo na kusisitiza kuwa hawawezi kuruhusu kipigo pamoja na kwamba matokeo hayatawapeleka kokote.
Katika usajili wa Yanga kwenye mashindano ya kimataifa, Yanga itawakosa nyota wake watano ambao walisajiliwa kucheza kwenye mashindano ya kimataifa msimu huu.
Wachezaji hao ni Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Hassan Kessy ambao wamesajiliwa na timu nyingine wakati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amestaafu na Vincent Bossou hayupo na timu hiyo.
“Wachezaji wengine wote waliosajiliwa watakuwepo kwenye mchezo huo, isipokuwa hao watano,” alisema Mwandila.
Yanga ambayo iliweka kambi mkoani Morogoro kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu sanjari na kujiweka fiti kwa mchezo huo wa kimataifa imerejea Dar es Salaam jana Jumamosi tayari kwa mchezo wao wa Jumapili.
“Timu iko katika kiwango bora, bila shaka tutautumia mchezo huo kwa ajili ya kujiweka tayari kwa msimu mpya wa Ligi Kuu,” alisema.
Kwenye kundi hilo, Gor Mahia inaongoza ikiwa na pointi nane sawa na USM Alger zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Rayon yenyewe ni ya tatu katika msimamo ikiwa na pointi tatu, ingawa bado ina mategemeo ya kufuzu kucheza robo fainali endapo itashinda mechi dhidi ya Gor Mahia na ile ya mwisho na Yanga nchini Rwanda huku ikiombea matokeo mabaya kwa yoyote kati ya Gor Mahia au USM Alger kwenye mechi zilizosalia.