Manchester City vs Man Utd ‘derby’ ya kukata na shoka

Manchester, England. Pambano la kukata na shoka katika Ligi Kuu England, linatarajiwa kufanyika kesho kati ya mahasimu wa mji wa Manchester, Man City dhidi ya Man United.

Hata hivyo, jeuri ya kuwa na mashabiki wengi zaidi imewafanya Man United kupuuzia pambano hilo kwa hoja kwamba Man City sio saizi yao, bali wapinzani wao wa jadi ni Liverpool.

Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Etihad kuanzia saa 1:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki utakuwa kama michezo mingine ya hivi karibuni inayozikutanisha Man City ikiwa katika kiwango bora huku Man United inayocheza soka ya wastani.

Man City itashuka dimbani ikiongoza Ligi hiyo kwa pointi 29 baada ya kucheza mechi 11 wakati Man United ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi 20 zote zikiwa zimecheza idadi sawa ya michezo.

Kuna jambo moja linaloongeza upinzani katika mchezo huo nalo ni upinzani uliopo baina ya makocha wa timu hizo ambao ulioanza tangu wakiwa nchini Hispania. Kocha wa Man City, Pep Guardiola, alikuwa akiinoa Barcelona, wakati Jose Mourinho wa Man United alikuwa akiinoa Real Madrid timu zenye nguvu na upinzani zaidi katika Ligi ya Hispania.

Aprili mwaka huu katika mechi ya marudiano ya msimu uliopita Mourinho na vijana wake licha ya kuingia katika mchezo huo wakiwa hawapewi nafasi kubwa ya kushinda kama ilivyo safari hii, waliiduwaza Man City walipoifunga mabao 3-2 kwenye Uwanja huo.

Timu hizo zinakutana zote zikitoka kushinda mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano iliyopita, Man City ikiirarua Shakhtar Donetsk 6-0 na Man United ikiwa ugenini mjini Turin ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Juventus.