Kinda hawa wako sokoni

Eliud Ambokile

Muktasari:

  • Makocha wa Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara, wameanza kupigana kumbo kuwania saini za baadhi ya wachezaji chipukizi waliocheza kwa kiwango bora katika mashindano hayo.
  • Dirisha la usajili limefunguliwa rasmi leo hadi Desemba 15 na klabu zina fursa ya kusajili wachezaji wapya kama hazijatimiza idadi inayotakiwa.

Dar es Salaam. Wakati dirisha dogo la usajili linafunguliwa rasmi leo, tayari wachezaji 11 chipukizi wamejiweka sokoni baada ya kuonyesha kiwango bora katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Klabu za Ligi Kuu ambazo hazijatimiza idadi ya wachezaji wanaotakiwa kwenye mashindano hayo zimeanza mchakato wa kuwania saini ya za nyota hao baada ya kuvutiwa na viwango vyao.

Kipindi hiki cha usajili kimekuwa kikiwaweka roho juu makocha wengi hasa ambao wameshindwa kuonyesha mafanikio katika mechi 14 za raundi ya kwanza.

Idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza safu ya ushambuliaji wamejiweka sokoni kutokana na ubora wao wa kufunga mabao wakishindana na wakongwe.

Chipukizi wenye nafasi ya kusajiliwa ni wale wanaocheza safu ya ushambuliaji kwa kuwa wana fursa ya kuziletea mafanikio klabu zao.

Eliud Ambokile amewashangaza wadau wa soka kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika kufunga mabao akimpiku mshambuliaji nyota wa kimataifa Emmanuel Okwi.

Ambokile anayeongoza wachezaji wanaochipukia vyema, anaongoza kwa kufunga mabao manane akimpiku Okwi mwenye saba.

Simba, Yanga na Azam zimeanza mchakato kuwania saini ya kinda huyo mwenye miaka 20 ambaye amekuwa chachu ya ushindi katika kikosi cha Mbeya City.

Kinda mwingine anayeinukia vyema ni Yahaya Zayd wa Azam ambaye licha ya umri mdogo wa miaka 20, ameingia vitani kusaka kiatu cha dhahabu msimu huu.

Kiwango chake bora kimemshawishi kocha wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Emmanuel Amunike kumpa nafasi katika kikosi chake.

Zayd aliyeongozana na Taifa Stars kwa mechi ya Lesotho, anaweza kukabiliwa na changamoto ya kuwania namba baada ya ujio wa Obrey Chirwa aliyejiunga na Azam.

Katika nyota wanaofanya maajabu msimu huu, huwezi kuweka kando jina la kinda mwenye miaka 18

Kelvin Nashon wa JKT Tanzania.

Kinda huyo ndiye mpishi mkuu wa timu hiyo anayecheza kwa kiwango bora katika nafasi ya kiungo. Ni mmoja wa vijana ambaye ni hazina kwa Taifa siku za usoni.

Kocha wa Coastal Union Juma Mgunda, humwambii kitu kuhusu beki wake wa kati Bakari Mwamnyeto ambaye amekuwa kisiki kwa washambuliaji wa timu pinzani.

Simba, Yanga na Azam kinda huyu mwenye miaka 21, anafaa kucheza katika timu hizo kutokana na uhodari wake wa kukaba.

Issa Abushehe ni chipukizi mwingine wa timu hiyo anayekuja kwa kasi, licha ya kuwa na miaka 18, ni kiungo anayetumia akili na huenda katika dirisha dogo akatimka kwa wagosi wa kaya.

Cliff Buyoya wa KMC ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kulimwa kadi nyekundu msimu huu, lakini hakukutetereka aliendelea kucheza kwa ubora ule ule hadi sasa licha ya kuwa na umri wa miaka 19 tu.

Buyoya aliyefunga bao moja kweye ligi, anatajwa na Kocha Etienne Ndayiragije ndiye mshambuliaji mwenye ushawishi wa kutengeza nafasi za mabao.

Simba na Azam hazitamsahau Charles Ilamfia wa Mwadui Shinyanga, ambaye amekuwa gumzo kwa makocha wa timu hizo baada ya kuzifunga kila moja msimu huu.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 22, tayari ana mabao matatu ambayo yanamuweka katika nafasi nzuri ya kushindana kuwania kiatu cha dhahabu.

Viwango bora vya chipukizi hao vimewaibua baadhi ya makocha akiwemo Mwinyi Zahera wa Yanga, anayewataja vijana hao ni moto wa kuotea mbali.

"Wachezaji wengi vijana  wamefanya vizuri na hiyo inaleta changamoto kwa wazoefu kupambana zaidi.Mfano Godfrey kama ataendelea kujituma basi atakuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania.Ana kasi na anajua nini afanye hivyo nitaendelea kumuamini na kumpanga kikosi cha kwanza"alisema Zahera.

Kocha wa Mbeya City, Ramadhani Nsanzurwimo amesifu viwango vya wachezaji chipukizi kwenye ligi na amewataka kutobweteka na mafanikio waliopata.

“Wameonyesha kiwango kikubwa, muhimu waongeze juhudi bado vijana wadogo na wana muda mrefu wa kucheza. Kama Eliud Ambokile amefanya vizuri kuwazidi hata wachezaji wa nje Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Herieter Makambo,” alisema Nsanzurwimo. 

Naye kocha wa zamani wa Cargo, Bandari na Yanga, Kennedy Mwaisabula amewataka wachezaji hao kutofanya makosa kukimbilia fedha katika kipindi hiki cha usajili ili kulinda vipaji vyao.

"Wengi wamecheza vizuri na kuwashangaza wengi, lakini ni muhimu kujua kabla ya kusajiliwa na timu kubwa wajifunze kutoka kwa wenzao mfano Marcel Kaheza, Adam Salamba na Mohammed Rashid wa Simba ambao hawapati nafasi ya kucheza,”alionya Mwaisabula.