#WC2018: Afrika njia panda Kombe la Dunia

Muktasari:

Vipigo ilivyopata Misri, Morocco na Nigeria kwenye mechi zao za kwanza, vimefanya wawakilishi hao wa Afrika katika fainali hizo kujiweka katika mazingira magumu ya kufuzu hatua ya 16 Bora ya mashindano hayo.

Dar es Salaam. Wakati Tunisia ikivaana na England leo saa tatu usiku kwenye mchezo wa Fainali za Kombe la Dunia, matokeo ya mechi za kwanza katika mashindano hayo yameziweka njia panda timu za Afrika.

Vipigo ilivyopata Misri, Morocco na Nigeria kwenye mechi zao za kwanza, vimefanya wawakilishi hao wa Afrika katika fainali hizo kujiweka katika mazingira magumu ya kufuzu hatua ya 16 Bora ya mashindano hayo.

Timu hizo zinalazimika kufanya kazi ya ziada katika mechi zilizobaki kumaliza katika moja kati ya nafasi mbili za juu kwenye makundi yao ili kuingia hatua ya mtoano, vinginevyo zitaanza mapema kufungasha virago kurejea nyumbani.

Nuksi kwa Afrika ilianza Ijumaa iliyopita baada ya Misri kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Uruguay ambacho kimeifanya timu hiyo kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi.

Namna pekee ambayo inaweza kuifanya Misri kufuzu hatua inayofuata ni kupata ushindi katika mechi mbili dhidi ya wenyeji Russia na Saudi Arabia.

Wawakilishi wengine wa Afrika, Morocco walijikuta wakipata mshituko baada ya kuangukia pua mbele ya Iran ilipofungwa bao 1-0.

Matokeo hayo yanailazimisha Morocco kusaka ushindi dhidi ya timu za Hispania na Ureno zilizotoka sare katika mchezo wa kwanza. Kinyume na matokeo hayo, Morocco itaaga mapema kwenye hatua ya makundi.

Mzimu wa matokeo mabaya kwenye mechi za mwanzoni uliendelea kuziandama timu za Afrika juzi usiku, baada ya Nigeria kujikuta ikichapwa mabao 2-0 dhidi ya Croatia. Ushindi katika mechi mbili zinazofuata dhidi ya Argentina na Iceland utaiwezesha Nigeria kupenya hatua ya 16 Bora.

Baada ya timu hizo tatu kupoteza mechi za mwanzoni, matumaini ya Afrika kwenye mechi za ufunguzi yameangukia kwa Tunisia inayocheza leo na England sanjari na Senegal ambayo itatupa karata yake kesho kukabiliana na Poland.

Katika timu hizo tatu ambazo tayari zimeshapoteza mechi zao za kwanza, ni Misri tu inayoonekana kuwa na nafuu ya kugeuza upepo kwa kuwa kundi lake linaonekana lina timu za wastani ambazo ikiongeza kasi inaweza kuibuka na ushindi na kusonga mbele.

Hata hivyo, Nigeria na Morocco zipo kwenye makundi yenye timu ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni.

Huu ni mwendelezo wa kufanya vibaya kwa timu za Afrika kwenye mechi za mwanzoni za hatua ya makundi ya Kombe la Dunia, matokeo ambayo mara kwa mara yamechangia kushindwa kufika hatua za juu kwenye mashindano hayo.

Katika Kombe la Dunia lililopita nchini Brazil, timu tano za Afrika zilivuna jumla ya pointi nne tu kati ya 12 ambazo zilipaswa kupata iwapo wawakilishi hao wangepata ushindi kwenye mechi hizo zote.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti makocha kadhaa nchini walisema kinachoziangusha timu za Afrika ni kujirudia kwa makosa ya siku zote zinapopata nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia.

Kocha msaidizi wa Singida United, Jumanne Chale, alisema; “Wenzetu wanafanya vizuri katika mashindano kutokana na mfumo mzuri, mfano nimefuatilia timu nyingi zilizoanza vizuri katika mashindano hayo zimetumia mfumo wa 4-3-1. Wanashambulia wote na wanarudi haraka kuzuia wanaposhambuliwa, hivyo waafrika wanatakiwa kubadilika ili kufanya vizuri,” alisema Chale.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema kilichozitokea timu za Afrika ni matokeo ya kawaida katika soka.

“Kuanza vibaya haina maana ndio mwisho wao. Kikubwa wanachotakiwa kufanya ni kuiba mbinu za wapinzani wao waliokutana nao katika michezo ya kwanza na kuzifanyia kazi,” alisema Katwila.

Kocha msaidizi wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’ alisema kupoteza hali ya kujiamini kumeziponza timu za Afrika kwa kuwa zimekuwa na mazoea ya kucheza soka ya kujisahau zinapomiliki mpira.