Bao lamtia 'mzuka' Edo Christopher

Muktasari:

  • Edo ameshafunga mabao mawili, moja alifunga dhidi ya Ndanda na la pili ni la jana Jumapili na Mtibwa Sugar, mechi iliyochezwa Uwanja wa Manungu, Morogoro.

BAADA ya straika wa Kagera Sugar, Christopher Edward 'Edo' kutupia bao la ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar, amesema limemwamsha na kumweka katika  ramani ya ushindani ili kuwa mmoja wa wafungaji bora.

Mpaka sasa Edo, ameshafunga mabao mawili, moja dhidi ya Ndanda na la pili ni la jana Jumapili na  Mtibwa Sugar, mechi ilichezwa Uwanja wa Manungu, Morogoro.

Amezungumzia furaha yake ya  kushinda ugenini, kwake ni faraja kuona ameisaidia timu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, tofauti na wangepoteza ama kuambulia pointi moja.

"Hata kama nimefunga bao moja dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini limeipa timu yangu hatua ya kupanda nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi, tutarejea nyumbani tukiwa na nguvu ya kuvuna pointi tatu ugenini,"alisema.

Edo ameongeza na kusema licha ya kuanza vibaya mechi za awali wanaamini watabadilika na kufanya vema kabla ya kutinga kwenye mzunguko wa pili wanaoamini una ushindani wa hali ya juu.

"Wengi walidhani kuanza kwetu vibaya ndiyo kwisha habari yetu, tumejifunza na tunaendelea kujifunza, hilo litatufanya tupambane hadi kieleweke,"anasema.