Alliance Girls yapigwa tafu

Muktasari:

Timu hiyo inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake itakayoanza mwishoni mwa wiki hii

Dar es Salaam. Timu ya soka ya wanawake ya Alliance Girls inayoshiriki Ligi ya Taifa ya wanawake leo imelamba udhamini mnono wa Shilingi 20 kutoka kampuni ya GF Trucks & Equipments inayohusika na biashara ya magari na vipuli vyake.

Udhamini huo wa aina yake umekuja siku tano kabla ya kuanza kwa ligi ya Taifa ya wanawake itakayoshirikisha timu 12 zilizogawanywa katika makundi mawili ambayo mechi zake zitachezwa katika vituo vya Arusha na Dar es Salaam.

Mkurugenzi mtendaji wa GF Trucks & Equipments, Imran Karmali alisema kampuni yake ina imeamua kugeukia soka la wanawake ili kuhamasisha wadau na makampuni mbalimbali kusapoti maendeleo yake kama wanavyofanya kwenye soka la wanaume.

"Udhamini huu kwa Alliance Girls unalenga katika kuthamini vipaji vya watoto wa kike kwani katika soka limekuwa ni kundi ambalo lina changamoto katika kufanikisha malengo yao ikiwa pia ni kutoa fursa na haki sawa kwa jinsia zote mbili.

Tunaomba makampuni na taasisi zingine kujitokeza kudhamini timu za wanawake au mashindano yao lengo likiwa ni kulikuza na kulitangaza soka la wanawake la nchi yetu," alisema Karmali

Mkurugenzi wa timu ya Alliance Girls, Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza, James Bwire ameishukuru kampuni ya GF Trucks & Equipments kwa udhamini huo wa kwanza kuwahi kutokea katika soka la wanawake.

"Uongozi wa Alliance unawashukuru sana GF Trucks kwa sababu wamekuja kutusaidia katika kipindi ambacho soka la wanawake linakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa udhamini na pia watu wamekuwa na mwamko mdogo nalo kulinganisha na soka la wanaume.

Tunaamini udhamini huu utakuwa chachu kwetu kufanya vizuri katika ligi ya taifa lakini pia naamini utafungua milango kwa kampuni, taasisi na hata watu binafsi kutoa sapoti kwenye mpira wa miguu wa wanawake," alisema Meya Bwire.

Alliance Girls ipo kundi B ambalo litatumia kituo cha Arusha linalojumuisha timu za Marsh Academy, Panama, Baobab Queens, Majengo Queens na Kigoma Sisters.