Amri akunjua makucha Mbao FC

Muktasari:

Akizungumza mjini hapa jana, Said alisema anavutiwa na usajili wa Mbao kwa kuwa imenasa saini za wachezaji watakaokidhi viwango katika kila idara.

Mwanza. Kocha wa Mbao Amri Said amesema ana matumaini Mbao FC itakuwa tishio katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Akizungumza mjini hapa jana, Said alisema anavutiwa na usajili wa Mbao kwa kuwa imenasa saini za wachezaji watakaokidhi viwango katika kila idara.

Kocha huyo alisema ana ndoto ya kuipa mafanikio Mbao katika Ligi Kuu ambayo msimu ujao itashirikisha timu 20 badala ya 16.

Beki huyo wa zamani wa Simba, alisema malengo yake ni kucheza mechi 10 za mwanzo katika Ligi Kuu bila kufungwa ili kujiweka katika nafasi nzuri ujao.

“Mambo yanakwenda vizuri na bahati nzuri viongozi wana kasi ambayo inanivutia na mipango yangu Ligi Kuu itakapoanza mechi kumi za mwanzo tushinde zote,”alisema Said aliyekuwa akifahamika kwa jina la Stam alipokuwa beki wa kati wa Simba.

Kauli ya Said inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Mbao Solly Njashi ambaye amesema klabu hiyo imemsajili kwa mkopo beki wa Azam, Karim Hamim.

Klabu hiyo imenasa saini za wachezaji watatu Elias Zamfuko (African Lyon), Peter Mwangosi (Njombe Mji) na Emmanuel Mtumbuka kutoka Dodoma FC.

Mwenyeki wa Klabu hiyo, Solly Njashi alisema usajili huo ni mapendekezo ya benchi la ufundi kuhakikisha timu inafanya vyema msimu ujao na uongozi umejipanga kutekeleza.

Msimu uliopita, Said alikuwa kochawa Lipuli ya Iringa.