Amunike aita nyota 9 wa kulipwa kuivaa Uganda

Muktasari:

  • Tanzania inasaka kufuzu kwa Afcon kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo 1980

Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike ameita wachezaji kikosi chake cha wachezaji 25 tisa wakiwa wanaocheza soka la kulipwa kujiandaa na mechi dhidi ya Uganda Septemba 8 wa kuwania kufuzu kwa mashindano ya Mataifa ya Afrika 2019, Cameroon.

Katika kikosi hiki cha kwanza Amunike ameita wachezaji wengi hata wale ambao waliotangaza kustaafu kuicheza timu huku akisisitiza kila mchezaji atakuwa na uhuru wa kuichezea timu ya Taifa Stars akionyesha uwezo katika klabu yake.

Wachezaji wanaocheza soka la kulipwa walioitwa ni pamoja na nahodha Mbwana Samatta (Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (Al Hilal Omdurman, Sudan), Shaban Chilunda, Farid Mussa (CD Tenerife, Hispania), Saimon Msuva (Diffa el Jadida, Morocco), Himid Mao (Petrojet FC, Misri), Abdi Banda (Baroka, Afrika Kusini), Hassan Ramadhani Kessy (Nkana FC, Zambia), Rashid Mandawa (BDF XI, Bostwana).

Akizungumzia kikosi chake Amunike alisema hii timu siyo ya mtu mmoja ni timu ya wachezaji wote kucheza, hakuna maajabu ambayo nitaweza kuyafanya zaidi ya kutengeneza mifumo mizuri ili timu iweze kufanya vizuri.

Licha ya kuibuka maneno kuhusu kuita wachezaji bila kuwaona, alitoa ufafanuzi kwamba alikuwa akiifuatilia Tanzania tangu Desemba na kugundua nini cha kufanya.

"Wachezaji wengi nilikuwa nawafuatilia, lakini nimeangalia wachezaji wengi kupitia video kwahiyo naamini kabisa nitakapokuwa nao kambini tutatengeneza kitu cha tofauti," alisema winga huyo wa zamani wa Barcelona na Nigeria.

Kikosi cha Taifa Stars kitakachoingia kambini ni Jumatatu ijayo: Makipa Aishi Manula (Simba), Mohammed Abdalrahman (JKU) Benno Kakolanya (Yanga).

Mabeki: Shomari Kapombe (Simba), Hassan Kessy (Nkana Rangers, Zambia), Gadiel Michael (Yanga), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Yanga), Aggrey Morris (Azam), Andrew Vicent (Yanga).

Viungo: Himid Mao (Petrojet, Misri), Mudathiri Yahya (Azam), Erasto Nyoni (Simba), Jonas Mkude (Simba), Saimon Msuva (Diffa Jadida, Morocco), Shiza Kichuya (Simba), Rashid Mandawa (DBF, Botswana), Farid Mussa (CD Tenerifa, Hispania), Hassan Dilunga (Simba), Feisal Salum (Yanga).

Washambuliaji: Mbwana Samatta (Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (Al- Hilal, Sudan), Shabani Chilunda (CD Tenerifa, Hispania), John Bocco (Simba) na  Yahya Zaydi (Azam).