Arsenal, Chelsea zatangulia 32 bora, Genk ya Samatta bado kidogo

Muktasari:

  • Timu za Arsenal na Chealsea zimefanikiwa kufuzu hatua ya mtoano wa michuano ya Europa ligi huku timu ya Genk anayochezea mtanzania Mbwana Samatta ikilazimika kusubiri hadi Novemba 29.

London, England. Licha ya Arsenal kubanwa na Sporting Lisbon ya Ureno na kulazimishwa sare ya bila mabao, timu hiyo imefuzu hatua ya mtoano ya Europa Ligi ikiwa na mechi mbili mkononi.

Sare hiyo imeiwezesha Arsenal inayoongoza kundi E, kufuzu kwani pointi kumi ilizovuna zinawezakufikiwa na Sportting pekee yenye pointi saba, lakini Vorskla Potava na FK Qarabag zenye pointi tatu kila moja, hazitaifikia hata kama zitashinda mecho zote mbili zilizosalia.

Nayo Chelsea ambayo imeendelea kufanya vema chini ya Kocha Maurizio Sarri, imefuzu hatua ya mtoano baada ya mshambuliaji wake Olivier Giroud, kuifungia bao pekee iliposhuka dimbani ugenini na kuizamisha BATE Borisov.

Chelsea iliyo Kundi L, imefikisha pointi 12 baada ya kushinda mechi zote inasubiri timu moja itakayoungana nayo kutinga 32 bora.

Timu ya MOL Vidi ina nafasi nzuri zaidi kwani ina pointi sita, wakati PAOK Salonika na BATE Borisov kila moja ina pointi tatu.

KR Genk ya Ubelgiji anayoitumikia nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, licha ya kuongoza Kundi I, lakini inalazimika kusubiri hadi Novemba 29 mwaka huu itakapoifuata Malmö FF kuona kama itatinga 32 bora au la.

Ingawa Genk inaongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi saba, lakini timu zote za kundi hilo zinaweza kufuzu kutokana na pointi kukaribiana sana.

Timu inayoshika nafasi ya pili nyuma ya Genk katika kundi hilo ni Sarpsbong yenye pointi tano, Malmo FF ina pointi tano pia wakati Besiktas ya Uturuki inayioburuza mkia katika kundi hilo ina pointi nne.

Hii inamaanisha kuwa hata timu inayoburuza mkia katika kundi hilo inaweza kufuzu hatua ya 32 bora iwapo itashinda mechi zake zilizosalia na timu nyingine zikapoteza au kutoka sare katika mechi hizo.

Aidha makundi mengine ambayo yana ushindani mkubwa na hakuna timu iliyojihakikishia kusonga mbele hadi sasa ni Kundi F, ambako Real Betis inaongoza kwa kuwa na point inane, ikifuatiwa na AC Milan na Olympiakos zenye pointi saba kila moja, F91 Dudelange inayoburuza mkia kwa kutoambulia pointi hata moja ndiyo haina nafasi.

Balaa kama hilo lipo pia katika wa Kundi G, katika kundi hili Villareal inaongoza kwa kuwa na pointi sita wakati Spatak Moscow ipo nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi tano sawa na Rangers wakati Rapid Vienna inayoburuza mkia ina pointi nne.

Nalo Kundi K mambo bado hayajakaa sawa kwani, FC Astana inayoongoza kundi hilo ina pointi nane sawa na Dynamo Kiev, wakati Rennes yenye pointi tatu bado inayo nafasi ya kufuzu iwapo itashinda mechi zake mbili zilizosalia na zilizo juu yake kupoteza.

Aidha katika kile kinachofahamika kuwa miujiza ya soka haitashangaza hata kama FK Jablonec inayoburuza mkia kwa kuwa na pointi mbili, ikifuzu na kuziacha zilizojuu zikiduwaa kwani ikishinda mechi zote mbili kwa idadi kubwa ya mabao na zilizo juu zikapoteza mechi zote.

Kundi A ndilo kundi pekee ambalo timu zote za kufuzu zimefahamika, ambazo ni Bayer Leverkusen na Zurich zenye pointi tisa kila moja.

Timu za Ludogorets na AEK Larnaca zenye pointi mbili kila moja, zikisubiri kukamilisha ratiba kwani hata zikishinda mechi mbili zilizobaki zitaishia pointi nane pekee.

Vinara wa kundi B timu ya RB Salzburg yenye pointi 12 imefuzu na kuziachia mchuano RB Leipzig na Celtic zenye pointi sita kila moja.

Ni miujiza ya soka pekee inayoweza kuivusha Rosenborg kutinga hatua ya 32, inapaswa kushinda mechi mbili zilizosalia kwa zaidi ya mabao 10-0 na kuombea timu mbili zilizo juu yake zipoteze mechi zote tena kwa idadi kubwa ya mabao ndipo ifuzu.

Kundi C, Zenit ST Petersburg inayoongoza ikiwa na pointi nane ina nafasi nzuri ya kufuzu kwani inahitaji pointi moja katika mechi mbili zilizosalia.

Kibarua kizito katika kundi hilo ipo kwa Slavia Prague inafuatia kwa kuwa na pointi saba na FC Copenhagen yenye pointi tano, ambapo yoyote itakayochanga vizuri karata zake katika mechi zijazo inaweza kufuzu, huku Bordeaux ya Ufaransa ikisubiri miujiza kuivusha.

Nalo Kundi H timu ya Frankfut ya Ujerumani imefuzu baada ya kujikusanyia pointi 12, ikifuatiwa na Lazio yenye pointi tisa, wakati Marseille na Apollon Limassol zenye pointi moja kila moja zikisubiri kutimiza wajibu.

 

&&&&&