DPP apewa tena jalada la kesi ya Aveva, Kaburu

Muktasari:

  • Washtakiwa hao wapo mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Dar es Salaam. Jalada la kesi inayowakabili vigogo wa klabu ya Simba akiwemo Rais wake, Evans Aveva na mwenzake limerejeshwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulipitia na kujiridhisha na upelelezi na mashtaka.

Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai alieleza hayo leo kwa Hakimu Mfawidhi, Victoria Nongwa.

Swai alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na jalada limerudishwa kwa DPP Kwa ajili ya kupitiwa na kwamba wanasubiri alipitie na kujiridhisha na upelelezi na mashtaka.

Wakati kesi hiyo ikitajwa mahakamani hapo alikuwapo Godfrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye ni Makamu wa Rais wa klabu ya Simba.

Swai alidai kuwa Rais wa klabu ya Simba hakufika mahakamani kwa sababu bado anaumwa na amepelekwa Hospitali katika kliniki yake.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, wakili wa utetezi, Steven Mwakiborwa aliomba kesi hiyo ipangiwe tarehe fupi.

Kesi imeahirishwa hadi Machi Mosi, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili  kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Washtakiwa hao, wanakabiliwa na Mashtaka matano ya uhujumu uchumi ikiwamo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha wa Dola za Marekani (USD) 300,000.

Washtakiwa hao wapo mahabusu kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.