Simba yatupwa kundi la kifo, Yanga kiulani Mapinduzi

Muktasari:

Mashindano hayo yanafanyika kwa lengo la kuenzi sherehe za Mapinduzi matukufu ya Zanzibar

Zanzibar. Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam wamepangwa kundi la kifo pamoja na Simba na URA ya Uganda huku Yanga ikipewa vibonde katika mashindano hayo yatakayoanza mwishoni mwa mwezi huu na kumalizika Januari 13, 2018, visiwani Zanzibar.

Katibu wa Kamatai ya Mashindano hayo, Khamis Abdalla Said amesema wamelazimika kupanga makundi mawili kutokana an uchache wa timu shiriki.

Akitangaza makundi hayo Kundi A, linaundwa na mabingwa watetezi, Azam FC, Jamhuri SC, Mwenge SC,  Simba pamoja na URA ya Uganda huku Kundi B likiwa na timu za JKU, Mlandege FC, Singida United, Taifa ya Jang’ombe, Yanga na Zimamoto.

Alisema kamati maalum ya mashindano hayo inatarajia kukutana hivi karibuni ili kupanga ratiba kamili ya michezo ya makundi yote, ratiba ambayo alidai kuwa inaonekana kusubiriwa kwa hamu na wapenzi na mashabiki wa soka visiwani humu.

“Tunataraji kutoa ratiba rasmi ya mashindano hayo hivi karibuni, kwani hivi sasa tunakamilisha hatua za mwisho ambapo kina jambo dogo tu limejitokoeza ndio maana tumechelewa ila ratiba itatoka mapema,”alisema .

Awaliwa kamati hiyo ilizitangaza timu yaYanga, URA ya Uganda, JKU, Zimamoto, Mlandege, Taifa ya Jang’ombe, Jamhuri, Mwenge, Simba na Azam pamoja na Shaba ndizo zinazoshiriki ila kutokana na timu ya Shaba  kukiuka taratibu za soka visiwani humu ilitolewa katika ratiba hiyo na kuingizwa Singida United.