Azarenka kuikosa US Open

Muktasari:

  • Azarenka aliyecheza fainali za US Open mwaka jana, alikosa nafasi hiyo baada ya kung’olewa katika raundi ya kwanza ya michuano ya Wimbledon na mchezaji chipukizi kutoka Jamhuri ya Czech, Karolina Pliskova.

New York, Marekani. Mchezaji bora wa zamani kwa wanawake Victoria Azarenka wa Belarus, anajuta kukosa tiketi ya kufuzu moja kwa moja kushiriki michuano ya US Open.

Azarenka aliyecheza fainali za US Open mwaka jana, alikosa nafasi hiyo baada ya kung’olewa katika raundi ya kwanza ya michuano ya Wimbledon na mchezaji chipukizi kutoka Jamhuri ya Czech, Karolina Pliskova.

Azarenka aliyefika fainali mbili za US Open alisema anasikitishwa sana na kiwango chake cha sasa namna kilivyoporomoka kiasi kwamba atalazimika kushinda mechi za mchujo ikiwa ni mara ya kwanza kuanzia hatua hiyo.

Azarenka nyota namba moja wa zamani na bingwa mara mbili wa michuano ya Australian Open, ameshika nafasi ya 108 kwa ubora katika viwango vilivyotolewa juzi ikiwa ni nafasi saba chini ya nafasi ya mwisho ya kufuzu moja kwa moja.

Chama cha tenisi ya kulipwa Marekani, kilitangaza juzi majina ya wachezaji waliofuzu moja kwa moja ambapo kwa wanaume mastaa wote watakuwepo ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki wote wakiwemo, Rafael Nadal, Roger Federer, Novak Djokovic, Andy Murray, Juan Martin del Potro na Marin Cilic.

Kwa wanawake waliofuzu ni pamoja na bingwa mara sita wa US Open, Serena Williams, dadake Venus Williams, bingwa mtetezi Sloane Stephens, Maria Sharapova na Samantha Stosur.