Barca yamtaka beki Blind wa Man United

Muktasari:

  • Miamba hiyo ya Hispania imekuwa na tatizo la kusumbuliwa na majeruhi wengi katika safu yake ya ulinzi

Barcelona inataka saini ya mchezaji kiraka Mholanzi wa Manchester United, Daley Blind akiwa mchezaji huru majira ya kiangazi msimu ujao.

Blind mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya beki na kiungo mkabaji, amebakiza mkataba wa miezi sita, hivyo ataondoka Man United akiwa mchezaji huru.

Mchezaji huyo huenda akaweka ngumu kutia saini mkataba mpya baada ya kukosa namba kikosi cha kwanza Man United.

Kocha wa Barcelona Ernesto Valverde anampigia hesabu mchezaji huyo mwenye miaka 27, licha ya kukosa namba chini ya kocha Jose Mourinho.

Kocha huyo amepanga kumtumia Blind kucheza beki wa kati kumrithi Javier Mascherano anayetarajiwa kujiunga na River Plate majira ya kiangazi.Blind ana uwezo wa kucheza beki wa kushoto, kati na kiungo mkabaji.