Beki Banda agoma kusaini mkataba Simba kisa ajiunge na Chipa United, Bidvest za Afrika Kusini

Muktasari:

Mchezaji huyo ameshamaliza mkataba wake na Simba, lakini uongozi wa klabu hiyo umempa ofa ya mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

 Beki wa Simba na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Abdi Banda amesema huenda asirudi nchini atakapoenda Afrika Kusini kushiriki mashindano ya Kombe la Cosafa.

Mchezaji huyo ameshamaliza mkataba wake na Simba, lakini uongozi wa klabu hiyo umempa ofa ya mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Banda alisema alishafanya makubaliano na viongozi wa timu Chipa United na Bidvest Wits FC, lakini uongozi wa Simba umemtaka kwenda Afrika Kusini akiwa ameshasaini mkataba mpya.

“Nina ofa tatu zikiwemo mbili za Chipa United na Bidvest Wits FC ambao walikuwa wananihitaji kwa muda mrefu, lakini uongozi wa Simba umenipa mkataba wa mwaka mpya na wamenitaka niusaini kabla ya kwenda Afrika Kusini,”alisema Banda, aliyejiunga na Simba 2014 akitokea Coastal Union ya Tanga.

Taifa Stars imealikwa kushiriki mashindano ya Cosafa inayoshirikisha nchini za Kusini mwa Afrika na imepangwa Kundi A na pamoja na Malawi, Angola na Mauritius.

Akizungumzia michuano ya Cosafa mchezaji huyo alisema itakuwa migumu, lakini ni fursa kwa wachezaji wa Tanzania kuonekana ikiwa watafanya vizuri.

“Ninaamini tunaweza kupambana na kufanikiwa, haya mashindano yana umuhimu mkubwa kwetu kama maandalizi ya kushiriki michuano ya Chan na Afcon, ni muhimu kwa wachezaji kuonekana,” alisema Banda.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx